Home Entertainment YANGA, WINGA BAMAKO MAMBO SAFI

YANGA, WINGA BAMAKO MAMBO SAFI

KWA mara ya pili Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi amekutana na winga Real Bamako ya nchini Mali, Cheickna Diakite na kufanya naye kikao cha siri.

Jana baada ya mchezo huo, kigogo wa Yanga alimwambia mwandishi wa gazeti hili kuwa, Diakite ni mchezaji mzuri ambaye amekuwa akimfuatilia tangu zamani kwa lengo la kumsajili kikosini hapo kwenye dirisha kubwa na anaamini watatumia fedha nyingi ili kumshawishi kuachana na mpango wa kwenda kucheza Ulaya na kutua Jangwani.

Aidha mmoja wa viongozi wa Bamako alisema mipango yao kwa sasa ni kumuuza Diakite Ulaya na kuna timu nyingi zimeonyesha nia hasa kutokana na uwezo ambao amezidi kuuonyesha winga huyo huku umri wake wa miaka 18 ukionekana kumruhusu kucheza soka kwa muda mrefu zaidi.

Sasa jana baada ya mechi kati ya Yanga dhidi ya Bamako ukiwa ni mchezo wa nne wa hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar ambao Yanga ilishinda mabao 2-0 Championi Ijumaa lilimshuhudia Nabi akizungumza na winga huyo.

Hicho ni kikao cha pili kocha huyo kufanya na winga huyo kwenye ambaye aliisumbua safu ya ulinzi ya Yanga tangu katika mchezo wa kwanza uliochezwa huko Mali.

Mtunisia huyo alitumia dakika zaidi ya nne kufanya mazungumzo na nyota huyo kabla ya kumruhusu kwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo uwanjani hapo.

Taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, Nabi yupo katika ushawishi mkubwa wa uongozi wa timu hiyo, kumsajili winga huyo katika usajili mkubwa wa msimu ujao.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, mabosi wa Yanga wapo katika mazungumzo na uongozi wa Bamako kwa ajili ya kuinasa saini ya winga huyo mwenye anayemudu kucheza namba 7, 10 na 11.

“Kocha Nabi anatumia michuano hii ya kimataifa kwa ajili ya kufanya skauti ya wachezaji, kwa yule atakayemvutia anafanya naye mazungumzo kabla ya kuuambia uongozi.

“Kati ya hao yupo huyo Diakite na Kinzumbi (Philippe) ambaye ni winga wa TP Mazembe aliyezungumza naye mara baadaya mchezo wa Shirikisho uliochezwa Uwanja wa Mkapa,” alisema mtoa taarifa huyo.

Nabi alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Hakuna nilichozungumza na Diakite zaidi ya kumpongeza kwa mchezo mzuri, ni mchezaji anayecheza vizuri katika nafasi yake.”

NA WILBERT MOLANDI, CHAMPIONI

Previous articleBEKI YANGA AITIKISA AFRIKA
Next articleKOCHA SIMBA AKILI NYINGI, MABOSI YANGA WASHTUKA