Home International KIMATAIFA NI MUDA WAKUONYESHA KAZI KWA VITENDO

KIMATAIFA NI MUDA WAKUONYESHA KAZI KWA VITENDO

KILE kipengele cha kutamba kuwa ni mkubwa kwa watani za jadi sasa kinapaswa kuonyeshwa kwa vitendo kutokana na mashindani ya kimataifa ambayo yapo mbele yao.

Simba wao wapo ndani ya Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi na wanatarajiwa kumenyana na Horoya Februari 11 ugenini na Yanga wao Februari 12 wana kete yao kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga itakuwa na kazi ya kusaka ushindi dhidi ya US Monastri hapa tunakuonyesha baadhi ya vipengele ambavyo wanafanya vizuri ndani ya ligi na vinapaswa kuonyeshwa anga la kimataifa namna hii:-

Wakali wa pasi

Ndani ya Simba wakali wa pasi kwenye ligi wamejaa kila kona ukianzia kwa mabeki ambapo Mohamed Hussein na Shomary Kapombe hawa wote wametengeneza pasi tanotano.

Kinara wa pasi kwa sasa kwenye ligi ni Clatous Chama akiwa nazo kibindoni 14 hii ni namba kubwa na inaonyesha uwezo wake kuwasoma wachezaji na kuwaelekeza ni mkubwa basi ni kazi yao kuhamishia yale yote kwenye anga za kimataifa.

Ukiwagusa Yanga ni Jesus Moloko mwenye pasi nne za mabao anafuatiwa na Aziz KI mwenye pasi tatu ndani ya ligi ujuzi wao uhamie kwenye anga za kimataifa katika kufanya kweli.

Mipira iliyokufa

Chama na Saidi Ntibanzokiza wanakimbiza kwenye mapigo huru ndani ya Simba huku pasi zake mbili kwenye mchezo uliopita alizotoa Chama ilikuwa ni kwa mapigo ya faulo huku Ntibanzokiza yeye akifunga kwa penalti mbele ya Mbeya City.

Yanga wao wanaye Aziz KI ambaye anawatesa kinomanoma makipa wa Bongo kuanzia Aishi Manula mpaka Jonathan Nahimana walikutana na balaa lake, pia yupo Djuma Shaban ambaye ni mtaalamu wa mapigo ya kona.

Balaa lao ambalo wanalifanya kwenye ligi muda mwingine kwa vitendo kuhamishia kwenye anga za kimataifa.

Ukuta chuma

Simba ni namba mbili kwa timu zilizotunguliwa mabao machache kwenye mechi za ligi ambayo ni 13 baada ya kucheza mechi 22. Yale makosa ambayo yametokea kwenye mechi zao ni muhimu kufanyia kazi ili kuwa bora.

Kwa upande wa Yanga hawa ni namba moja kwa timu iliyotunguliwa mabao machache ambayo ni 10 ikiwa na ukuta wenye maelewano mazuri ambayo yanahitajika kuendelea na kwenye mechi za kimataifa.

Watembeza mikato tahadhari

Mzamiru Yassin, Ismail Sawadogo, Sadio Kanoute ni miongoni mwa mastaa wanaotembeza mikato ya kimyakimya na kwenye anga la kimataifa muhimu kuwa na tahadhari ili kutopata kadi.

Yanga mkali wao ni Zawad Mauya,Khalid Aucho naye yumo katika kuzidisha ule uimara wa kupata ushindi ni lazima kuwa makini kwenye ukabaji na kujilinda.

Makipa kimataifa

Aishi Manula ana maswali mengi yakujibu hasa kwenye upande wa mapigo huru ambayo yamekuwa yakimshinda kwenye mechi za hivi karibuni.

Mchezo uliopita dhidi ya Singida Big Stars alitunguliwa bao kwa pigo la faulo na Bruno Gomez kazi bado haijaisha kimataifa umakini unahitajika

Djigui Diarra yupo zake ndani ya Yanga akiwa kwenye ubora ndani ya ligi ambapo mechi 9 mfululizo wakati Yanga ikishinda yeye katunguliwa mabao kwenye mechi moja pekee dhidi ya Azam FC.

Kujiamini kwake na kuendeleza ule ubora kwenye anga la kimataifa ni muhimu ili kutimiza majukumu yake.

Washambuliaji

Juma Mgunda, kocha msaidizi wa Simba amesema kuwa wanatengeneza nafasi nyingi kwenye mechi zao lakini hawazitumii zote.

Jambo hili nalo ni muhimu kwa mastaa wa Simba ikiwa ni pamoja na John Bocco, Habib Kyombo, Jean Baleke kuongeza umakini eneo hilo.

Cedrick Kaze, kocha msaidizi wa Yanga pia amesema kwenye mechi za kimataifa nafasi kutengeneza ni ngumu hivyo ikipatikana ni lazima itumike kwa umakini.

Previous articleMERIDIANBET YAGAWA NGUO KWA BODABODA JIJINI DAR ES SALAAM
Next articleAZAM FC YAANZA MATIZI KUMVUTIA KASI MNYAMA