MWISHO WA MJADALA, MOROCCO INATOSHA AFCON 2025

    Saleh Ally, Casablanca

    NOVEMBA mwaka jana wakati wa Fainali za Ligi ya Mabingwa ya Wanawake iliyofanyika nchini hapa, Rais wa Caf, Patrice Motsepe aliwakaribisha Morocco kuingia kuomba kuandaa mashindano ya Afcon mwaka 2025.

    Motsepe hakuwa na choyo katika maneno yake, alieleza wazi ambavyo amekuwa akivutiwa na Morocco inavyojipanga katika masuala kadhaa ya soka lakini pia kusaidia maendeleo ya soka la Afrika katika nchi mbalimbali.

    Wakati huo, FAR Rabat ya Morocco ilikuwa imeingia fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya mabingwa dhidi ya mabingwa watetezi wakati huo, Mamelodi Sundowns ambao waliingo’oa Simba Queens ya Tanzania kuingia fainali.

    Motsepe ambaye ni mmiliki wa Mamelodi, alishuhudia vijana wake wakivuliwa ubingwa na Morocco ikajiweka katika njia sahihi ya ukubwa katika soka la wanawake barani Afrika baada ya mapambano ya muda mrefu.

    Kwa wanaofuatilia soka, hakuna asiyejua mwendo bora wa Morocco katika soka ukianza na vijana, sasa wanawake na timu yao kubwa.

    Wana rekodi mpya ya kuwa timu iliyofanikiwa zaidi. Katika Kombe la Dunia baada ya kuingia nusu fainali ya Kombe la Dunia katika michuano iliyofanyika Qatar mwaka jana.

    Usisahau wakati FAR Rabat ni mabingwa wa wanawake Ligi ya Mabingwa Afrika, vigogo Wydad Casablanca ni mabingwa wa upande wa wanaume.

    Kabla ya hapo walikuwa mabingwa wa CHAN na walipoteza ubingwa baada ya kutokwenda Algeria na Senegal wakalibeba kombe wakiwatwanga wenyeji Algeria.

    Tukubali kwanza, kama kimafanikio kwa mataifa ya Kaskazini mwa Afrika na baadaye Afrika nzima kwa sasa, Morocco wako mbali.

    Wako mbali kwa nje unaweza kujiuliza maswali mengi. Sasa mimi niko ndani, niko jikoni, nakuambia nisikilize. Hawa jamaa wako vizuri na wamejipanga kwa miaka mingi.

    Kumbuka wameishaomba kuandaa Afcon 2025 na wapinzani wao ni Zambia, Benin, Nigeria, Benin na Algeria lakini kama ni ukweli, uwazi basi tuwe wazi kwamba Morocco wanastahili kushinda.

    Nasema wanastahili kwa kuwa nimejionea kiwango cha maandalizi yao na hasa miundombinu.

    Kwanza utazungumzia viwanja, binafsi nimetembelea viwanja vitano katika safari ndefu na ya kuchosha lakini hakika nimejifunza mambo mengi sana.

    Ukiangalia mikoa mitano niliyotembelea ya Agadir, Fez, Rabat, Tangier na Marrakech. Viwanja vyote vinastahili kuandaa Kombe la Dunia chini ya Fifa au Kombe la Mataifa Afrika chini ya Caf.

    Viwanja vina ubora sahihi na vimepitishwa. Viko sehemu sahihi na vinafikika kwa uhakika ikiwemo kutoka katika mikoa jirani.

    Grande Stade de Marrakech:

    Huu uko katika jiji la kitalii la Marrakech na uwezo wake ni kubeba watu 45,240. Uwanja huu ni wa kisasa kabisa na uko katika mazingira bora na umekidhidi vigezo vyote vya Fifa na Caf.

    Stade Ibin Batuta:

    Mji wa Tangier, uko Kaskazini mwa Morocco, ndio mji ulio na mlango wa Gilbratar, ndani ya saa moja kwa boti unakuwa Hispania. Kipindi hiki kuna baridi sana na hapa ndipo unapatikana uwanja huu wenye uwezo wa kubeba watazamaji 65,000, maana yake ni mkubwa kuliko Benjamin Mkapa.

    Katika michuano ya Kombe la Dunia ya klabu, Uwanja huu ulitumika katika mechi Al Ahly dhidi ya Auckland City ya New Zealand na baadaye Al Hilal ya Saudi Arabia ikiitwanga Flamengo ya Brazil mabao 3-2 na kutinga fainali,

     Adrad Stadium:

    Uwanja huu unabeba watazamani 45,480, uko katika mji mzuri wa Agadir, Kusini mwa Morocco. Naweza kusema ni kama Mtwara ya Morocco, hakika ni kati ya viwanja vinavyovutia sanasana.

    Ukiuona huwezi kuamini uwanja huo uko eneo hilo kutokana na ubora wa viwango vyake ndani, lakini mazingira sahihi kabisa. Muunganiko wa Agadir na mikoa mingine, barabara nyingi ni mpya na za uhakika kabisa.

    Fez Stadium:

    Uwanja huu uko katika mji wa kihistoria wa Morocco unaoitwa Fez. Mji mkongwe wenye kumbukumbu nyingi za nchi hiyo na unabeba watu 45,000. Ninaamini huu ni mmoja wa viwanja bora si Morocco tu, Afrika kabisa.

    Prince Moulay Abdellah:

    Uwanja huu umetumika kwa mechi moja ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la klabu, Real Madrid wakiwavaa vigogo wa Afrika, Al Ahly, mechi ya mshindi wa tatu na fainali.

    Unabeba watu 52,000, hakuna ubishi kuhusiana na ubora wake. Kuaminika kwa fainali ni jibu tosha kabisa kwamba ni bora na ukumbuke fainali mbili za michuano hiyo hapo nyuma zilipigwa Ibn Batouta pale Tangier, lakini sasa mambo yamehamia Prince Moulay Abdellah.

    Nigeria, majirani zetu Zambia, Benin wanahitaji kujipanga kama ambavyo Morocco imetulia kwa muda mwingi ikijijenga lakini Algeria nao wanaweza kupata muda wa kujijenga baada ya kuwa siku chache wameandaa michuano ya vijana lakini Chan.

    Ukiangalia kwa usahihi, safari hii ni Morocco na ninaamini kama ambavyo wamekuwa wakijigamba, wataandaa mashindano ya Afcon ya kihistoria, ninaamini inawezekana.

     Katika viwango vya Fifa, Morocco inashika namba 11 duniani kwa ubora.

    Previous articleWAARABU WANAKUFA MAPEMA, SIMBA YAWEKA MKAKATI MZITO CAF
    Next articleYANGA HAWANA JAMBO DOGO WAANZA MAZOEZI