>

MOROCCO WAMETISHA KOMBE LA DUNIA

TIMU ya Taifa ya Morocco imetinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwenye historia baada ya kushinda katika hatua ya 16 hatua bora kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Hispania, Qatar 2022.

 

Matokeo haya yanamaanisha kwamba Morocco ambayo ni timu pekee kutoka Afrika iliyobaki kwenye mashindano haya itacheza na Ureno hatua ya robo fainali, Jumamosi, Desemba 10.

Morocco ilishinda kwa penalti 3-0 Hispania huku nyota anayekipiga ndani ya Paris Saint-Germain, (PSG)  Achraf Hakimi alifunga penalti ya ushindi kwa mtindo wa Panenka baada ya mchezo huo kukamilisha jumla ya dakika 120 kwa timu zote kutoshana nguvu bila kufungana.

Abdelhamid Sabiri na Hakim Ziyech hawa walifunga penalti za ufunguzi kwa Morocco huku kipa wao Yassine Bono akiokoa michomo ya Carlos Soler na Sergio Busquets, wakati Pablo Sarabia alikosa penalti yake kwa upande wa Hispania.

Timu zote mbili zilikuwa na nafasi ya kushinda mchezo huo kwenye dakika 90 za mwanzo na hata zile 30 za nyongeza lakini bahati haikuwa kwao huku Morocco wao ikionekana kwamba walikuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

Licha ya kuwa kwenye umiliki mzuri wa mpira Hispania walikuwa wabovu kwenye kumalizia nafasi jambo lililopelekea kuongezwa muda wa nyongeza na walifanikiwa kupiga shuti moja pekee lililolenga lango dakika 45 za mwanzo ikiwa ni rekodi mbovu tangu 1966.