BAO la kiungo wa Yanga, Feisal Salum dakika ya 89 limebutua fuko la shilingi milioni 20 ambazo waliahidiwa wachezaji wa Prisons kubeba ikiwa watashinda mchezo huo na kama wangeambulia sare milioni 10.
Ahadi hiyo ilitolewa na Ofisa Masoko wa Kampuni ya Silent Ocean, Mohamed Kamilagwa ikumbukwe kwamba hao ni wadhamini wakuu wa Tanzania Prisons.
Desemba 4,2022 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 1-0 Prisons hivyo fuko la milioni 20 limeyeyuka kwa bao la kiungo huyo aliyetumia pasi ya Farid Mussa ndani ya 18.
Baada ya bao hilo kiungo Feisal alisema kuwa waliingia kwenye mchezo huo kwa tahadhari na kutengeneza nafasi ili washinde jambo lililofanikiwa.
“Unaona kwenye mchezo wetu tulikuwa tunatengeneza nafasi ili tushinde hata mimi nilikuwa nikifanya majaribio ya nje ya 18 ili kufunga lakini haikuwezekana.
“Ambacho niliona itakuwa ni mpango wa pili ni kuingia ndani ya 18 hilo lingetupa penalti kama tungechezewa faulo ama bao kama ambavyo imetokea na tumeshinda mchezo wetu,”.
Feisal amefunga mabao matano akiwa amecheza mechi 12 ndani ya ligi msimu wa 2022/23.