Home Uncategorized SERENGETI GIRLS WAPAMBANAJI WANASTAHILI PONGEZI

SERENGETI GIRLS WAPAMBANAJI WANASTAHILI PONGEZI

TIMU ya Taifa ya Wasichana ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Girls, jana Jumamosi iliyaaga mashindano ya Kombe la Dunia Wanawake U17 baada ya kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Colombia, lakini wametuhesimisha Watanzania.

Kikosi hicho cha Bakari Shime, kilimaliza mechi hiyo ya robo fainali kikiwa tisa uwanjani kufuatia wachezaji wawili kuonyeshwa kadi nyekundu.

Alianza Zainabu Mohamed ‘Dudu’ kuonyeshwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza, kabla ya nahodha Noela Luhala kuonyeshwa kipindi cha pili.

Serengeti Girls imeondoshwa kwenye michuano hiyo ikiwa ni timu iliyooneshwa kadi nyekundu nne.

Wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu ni mshambuliaji Neema Paul, aliyepewa kadi hiyo kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Japan, Tanzania wakipoteza kwa mabao 4-0.

Licha ya kuondolewa kwenye mashindano, benchi la ufundi la timu hiyo limeweza kufikia malengo waliyojiwekea ya angalau kufika hatua ya robo fainali kutokana na ugeni na uchanga wa kushiriki mashindano hayo.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza Tanzania inashiriki mashindano hayo makubwa yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Ikumbukwe kuwa, Serengeti ilitinga hatua ya robo fainali baada ya kumaliza wa pili Kundi D, ikitoka kuwachapa Ufaransa mabao 2-1, kisha sare ya 1-1 dhidi ya Canada. Mechi ya kwanza ilifungwa 4-0 na Japan.

Previous articleBOFYA MARA MOJA TU, UIBUKE MSHINDI SIMU MERIDIANBET
Next articleSIMBA WABAINISHA WAMECHOKA KUFUNGWA NA YANGA