WAKALI WAKIANZIA BENCHI LAZIMA WAFANYE KWELI

MIPANGO ya ushindi kusukwa inaanza kwa wachezaji wale waliopo ndani ya uwanja na wale wanaokaa benchi kusoma mchezo unavyoendelea.

Ndani ya ligi msimu wa 2022/23 wapo mastaa ambao wamekuwa wakali wakianzia benchi kwa kuwa walipoingia walifanikiwa kubadilisha namba kwenye ubao.

Hapa tunakuletea baadhi ya nyota ambao wamekuwa na makali wakianzia benchi namna hii:-

Feisal Salum

Kiungo huyu wa Yanga msimu huu katupia mabao mawili kwenye ligi na ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Azam FC uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Septemba 6,2022, Yanga 2-2 Azam FC, akitokea benchi alitumia dakika 45 alichukua nafasi ya kiungo Dennis Nkane alipachika mabao mawili dakika ya 57 na 77 akitumia mguu wa kulia akiwa nje ya 18.

Nickson Kibabage

Nyota huyu wa Mtibwa Sugar kwenye mechi mbili alikuwa mkali akianzia benchi kwa kuwa mechi hizo alifunga bao mojamoja.

Alianza kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC, Uwanja wa Mkapa, Agosti 15,2022 alipachika bao dakika ya 80 pia kwenye mchezo dhidi ya Ihefu alipachika bao moja dakika ya 82,  Septemba 7, Uwanja wa Manungu

 

Aziz KI

Kiungo huyu mshambuliaji wa Yanga alipachika bao lake la kwanza ndani ya ligi mbele ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Mkapa.

Mchezo huo ulichezwa Septemba 13,2022 alianzia benchi na alichukua nafasi ya kiungo Feisal Salum na alipachika bao lake la kwanza dakika ya 90 akiwa nje ya 18.

Mayele

Mshambuliaji huyu wa Yanga kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union alianzia benchi na alitumia dakika 35 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ubao uliposoma Coastal Union 0-2 Yanga.

Fiston Mayele alipachika bao moja dakika ya 67 na kuwafanya wasepe na pointi tatu jumlajumla.

Dejan Georgijevic

Mzungu wa Simba kwenye ligi katupia bao moja ilikuwa mbele ya Kagera Sugar ambapo ilikuwa ni zama za Zoran Maki ilikuwa ni Agosti 20,2022 Uwanja wa Mkapa.

Katika mchezo huo Dejan alitumia dakika 24, alichezewa faulo moja huku akikokota mpira mara mbili huku akitoa jumla ya pasi 7.

Okra

Agustino Okra staa wa Simba kibindoni ana bao moja alifunga dhidi ya Geita Gold ilikuwa Uwanja wa Mkapa,kwa pigo la faulo.

Alipachika bao hilo dakika ya 37 kwa mguu wa kushoto akiwa nje ya 18 baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Jonas Mkude.

Habib Kyombo

Mshambuliaji wa Simba, Habib Kyombo bao lake la kwanza aliwatungua KMC ilikuwa Uwanja wa Mkapa kwenye sare ya kufungana mabao 2-2, alipachika bao hilo dakika ya 89.

Seleman Ibrahim

Nyota huyu wa Geita Gold alipachika bao kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Septemba 6, Uwanja wa Kirumba kwenye sare ya kufungana bao 1-1, alianzia benchi na alipachika bao dakika ya 74.

Matheo Anthony

Mshambuliaji namba moja wa KMC, Matheo Anthony mwenye mabao manne, alipachika bao moja akitoka benchi ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Simba uliochezwa Uwanja wa Mkapa Septemba 7 dakika ya 48.

Chanzo Spoti Xtra mwandishi Dizo Click.