Home Sports MTANZANIA IBRA CLASS ATAMBA KUMDUNDA MMEXICO

MTANZANIA IBRA CLASS ATAMBA KUMDUNDA MMEXICO

BONDIA nyota wa Tanzania, Ibrahim Class ametamba kumchapa mpinzani wake Gustavo Pina Melgar kutoka Mexico katika pambano la kimataifa lililopangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City.

Pambano hilo limeandaliwa na Kampuni ya MO Boxing, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo chini ya mfanyabiashara maarufu, Mohammed Dewji.

Class amesema kuwa baada ya kukaa nje ya ulingo kwa muda mrefu, ameamua kurejea kwa kasi kwa lengo la kutwaa mikanda mbalimbali ya ngumi za kulipwa nchini.’

Amesema kuwa amejiandaa vyema kwa ajili ya pambano hilo na hatamdharau mpinzani wake kwani anaamini naye amekuja kwa ajili ya ushindi.

“Najua Melgar ni bondia mzuri lakini si kwa kufikia kwangu, nimejiandaa vyema na nimuonyesha jinsi gani Tanzania ina mabondia wazuri na wenye vipaji vikubwa,” amesema Class.

Kwa upande wake, Melgar amesema kuwa amekuja kusaka ushindi ili kuboresha rekodi yake katika ngumi za kulipwa.

Mratibu wa pambano hilo kutoka MO Promotion Ahmed Seddiqi amesema kuwa maandalizi yamekamilika na ambapo kutakuwa na mapambano sita ya utangulizi.

 Pambano la kwanza la utangulizi litakuwa kati ya bondia nyota wa Ghana, Alfred Lamptey ambaye atapambana na bondia Abraham Ndauendapo kutoka Namibia huku Juma Choki akizichapa na bondia wa kutoka Mexico Jose Hernandez ambapo bondia kutoka Kenya Nicholas Mwangi atapimana ubavu na Emmanuel Mwakyembe wa Tanzania.

 Pambano lingine litakuwa baina ya bondia Sameer Anwar dhidi ya Adam Mrisho huku Mwinyi Mzengela akizichapa na Sabari J na pambano lingine litakuwa baina ya Lulu Kayage dhidi ya Sadra Mohamed.

Mapambano hayo yamedhaminiwa na kampuni ya Azam TV, Boxer, MO XTRA, Mlimani City, KCB Bank, White Sands Resorts, Bajaj na OTAPP.

Kwa upande wake, Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa benki ya KCB, Christine Mnyenye amesema kuwa wanajisikia fahari kubwa kudhamini mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.

“Tunajisikia fahari kubwa kudhamini mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini ikiwa ni mara yetu ya kwanza, tutatumia mchezo huu kutambulisha huduma yetu mpya ya bima na kuwaomba wadau wa ngumi za kulipwa na watu wengine kujiunga nayo ili kujiwekea kinga na majanga mbalimbali,”amesema Mnyenye.

Previous articleWAKALI WAKIANZIA BENCHI LAZIMA WAFANYE KWELI
Next articleVIDEO: ULIMSKIA CEO MPYA WA YANGA? NENO LAKE LA KWANZA HILI HAPA