MWENDO wa kuwania kufuzu CHAN kwa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars umegotea Uganda baada ya kufungwa mabao 3-0 na kufanya itolewe kwa jumla ya mabao 4-0.
Mchezo wa leo Stars ilikuwa na mzigo wa kusaka mabao zaidi ya mawili na kupambana kujilinda wasifungwe jambo ambao liliweza kudumu katika dakika 14 za mwanzo pekee.
Mabao ya mchezo wa leo Septemba 3,2022 nchini Uganda, Uwanja wa St Marys yamefungwa na Moses Waigwa dakika ya 16 kwa mkwaju wa penalti, Basangwa dakika ya 52 na Rodgers Marco dakika ya 75.
Safu ya ushambuliaji ya Stars inayoongozwa na John Bocco jitihada zake za kusaka bao la kufuta machozi zilikwama kutokana na umakini wa kipa wa Uganda pamoja na safu ngumu ya ulinzi ya wapinzani.
Ni mchezo wa kwanza kwenye kuwania CHAN Stars kufuzu 2022/23 kipa Aishi Manula kutunguliwa mabao matatu.
Umakini wa safu ya ulinzi ya Stars inayoongozwa na Bakari Nondo na Mohamed Hussein, Kibwana Shomari ulikuwa ukipata tabu kutokana na kasi ya viungo na washambuliaji wa Uganda kuwapa presha mara kwa mara.