Home Uncategorized WAMEANZA MSIMU KWA MAJANGA MASTAA HAWA

WAMEANZA MSIMU KWA MAJANGA MASTAA HAWA

TAYARI mbio za kusaka ushindi kwenye Ligi Kuu Bara zinaendelea huku wachezaji wengine wakianza kwa majanga ya hapa na pale hali inayowafanya wasiwepo kwenye mechi za ushindani.

Wapo wengine ambao walianza msimu lakini majukumu waliyopewa kwao yaliwapa matokeo tofauti na kile ambacho wengi walikuwa wanatarajia.

Hapa tunakuletea baadhi ya mastaa ambao wameanza msimu kwa majanga namna hii:-

Abdul Seleman

Ingizo jipya ndani ya Azam FC akitokea kikosi cha Coastal Union alikuwa na kikosi nchini Misri kwenye maandalizi ya msimu wa 2022/23, aliporejea Bongo kwenye mazoezi aliweza kupata majeraha ambayo yamemuweka nje kwa sasa.

Aliitwa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kujiaandaa na mchezo dhidi ya Uganda lakini hakucheza kwa kuwa alikuwa chini ya uangalizi wa madaktari.

Aaron Kalambo

Nyota huyu ni kipa namba moja wa Dodoma Jiji yeye majanga yake ni kuokota mabao mengi nyavuni ambayo ni matano kwenye mechi tatu, ile ya kwanza alifungwa mabao 3 dhidi ya Mbeya City na alifungwa mabao 2 dhidi ya Tanzania Prisons.

Erasto Nyoni

Kiraka wa Simba hayupo kwenye kikosi cha timu hicho ambacho kimeweka kambi kwa muda nchini Sudan kutokana na kutokuwa sawa kiafya.

Kwa mujibu wa kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema kuwa nyota huyo anasumbuliwa na malaria.

Nyota huyo hajapata bahati ya kuweza kucheza kwenye mechi mbili za ligi ambazo Simba imecheza ilikuwa dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar.

Ibrahim Ally

Nyota huyu wa Namungo kwenye mchezo wake wa kwanza wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar alipewa jukumu la kupiga penalti mbele ya Mtibwa Sugar alipata majanga kwa kushindwa kumtungua Farouk Shikalo.

Mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Mkapa na ubao ulisoma Namungo 2-2 Mtibwa Sugar.

Mayele

Fiston Mayele mwenye mabao mawili ndani ya ligi alikwama kufunga penalti mbele ya Polisi Tanzania baada ya kipa kuweza kuokoa pigo hilo kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Mmanga

Mohamed Mmanga, nyota wa Polisi Tanzania alianza na majanga kwenye mchezo wake wa kwanza wa ligi dhidi ya Yanga kwa kuonyeshwa kadi mbili za njano dakika ya 44 na 88 jambo lililopeleka kuonyeshwa kadi nyekundu ya kwanza msimu wa 2022/23.

Jesus Moloko

Kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abedi nyota huyu alipata maumivu ambayo yalimfanya ashindwe kuyeyusha dakika 90.

Kabla ya kutoka alitoa pasi moja ya bao kwa kiungo Bernard Morrison dakika ya 4 na alitumia dakika 25 nafasi yake ilichukuliwa na Dickson Ambundo.

Nado, Ajibu,Chilunda

Mastaa hawa watatu wa Azam FC hawakuwa kwenye mpango wa kikosi cha timu hiyo kilichoikabili Taifa Jango’ombe kwenye mchezo wa kirafiki ambao ulikamilka kwa timu hizo kutoshana nguvu bila kufungana.

Idd Suleima, ‘Nado’ huyu alikuwa nje kwa muda tangu msimu uliopita akitibu majeraha yake, Ibrahim Ajibu na Idd Chilunda walipata maumivu hivi karibuni.

Kutoka Spoti Xtra imeandikwa na Dizo Click.

Previous articleWACHEZAJI STARS KAZI IPO KWENU KUJITUMA KUTAFUTA MATOKEO
Next articleVIDEO:JEMBE AWATAJA WATAKAOTEMWA SIMBA