MKUU wa Mkoa wa Tabora, Dk. Batilda Buriani ametoa hundi kwa vyama vya Ushirika (AMCOS) mkoani Tabora ikiwa ni sehemu ya fidia ya hasara ya mazao iliyotokana na kuwepo kwa mvua kubwa katika msimu wa 2021/2022.
Fedha hizo zimetolewa kupitia huduma ya Bima ya mazao ya Benki ya NBC ambayo inatoa kinga dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kama ukame, vimbunga, wadudu na mafuriko.
Inakuwa ni kwa mara ya kwanza nchini, wakulima wa zao la tumbaku mkoani Tabora kulipwa fidia na Benki ya NBC kufuatia hasara waliyoipata kutokana na uharibifu wa mazao yao baada ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika msimu uliopita.
Fidia hiyo imelipwa kupitia mpango wa Bima za Mazao wa Benki ya NBC.
Katika mpango huo, Vyama vinne vya Ushirika (AMCOS)ya Insolelansabo,Muloku, Ngulu Moja na Isenegezya vimepewa zaidi ya shilingi milioni tisa, kufidia hasara iliyosababishwa na kuwepo kwa kiwango cha juu cha mvua na hivyo kuharibu mazao na kusababisha hasara kwa wakulima hao.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi ya fidia kwa vyama hivyo, Mkurugenzi wa Wateja wadogo wa Benki ya NBC, Elibariki Masuke amesema fidia hiyo imetolewa kupitia mpango wa bima kwa wakulima ambayo inawalinda dhidi ya hasara zinazosababishwa na athari za hali ya hewa kama vile ukame, vimbunga, wadudu,mvua ya mawe na mengineyo.
“Kwa msimu wa mwaka huu kupitia vyama ambavyo vilikopeshwa na Benki ya NBC katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Shinyanga, wakulima waliweza kupata bima ya Kilimo ambayo iliwawezesha kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali,” amesema.
Ikumbukwe kwamba NBC pia kwenye sekta ya michezo wapo pia kwa msimu wa 2021/22 walikuwa ni wadhamini wakuu ambapo Yanga waliweza kutwaa ubingwa.