>

CR 7 HAUZWI KOCHA MANCHESTER UNITED ATHIBITISHA

KOCHA wa Manchester United raia wa Uholanzi Eric Ten Hag amewaambia Waandishi wa Habari kuwa mshambuliaji wa klabu hiyo Cristiano Ronaldo hauzwi.

Ten Hag ameyasema hayo kufuatia kuwepo kwa tetesi zinazomuhusisha nyota huyo kutimka katika viunga vya Old Trafford kufuatia klabu hiyo kutoshiriki katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya maarufu kama UEFA.

“Hajaniambia kuhusu hilo, nimesoma lakini kama nilivyosema, Cristiano hauzwi, yupo katika mipango yetu na tunataka kupata mafanikio pamoja.

“Tumepanga kuwa na Ronaldo kwenye msimu huu ni hivyo tu. Najiandaa kufanya naye kazi.

“Nimeongea naye kabla ya kuwa hapa. Nimekuwa na mazungumzo naye na yalikuwa mazungumzo mazuri.”

Ronaldo ambaye ni mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa wa muda wote hajasafiri pamoja na klabu hiyo kwenye maandalizi ya msimu mpya kuelekea nchini Thailand kutokana na kile kinachosemekana ni kuwa na matatizo ya kifamilia.

Moja ya klabu ambayo inahusishwa na kutaka saini ya mchezaji huyo ni Chelsea ambayo tajiri wake Todd Boehly anamtazama Ronaldo kama sehemu ya nyota wenye mvuto na thamani kubwa kibiashara.