NGUVU IWE KUBWA MAANDALIZI KOMBE LA DUNIA

    TAYARI mambo yameshakuwa hadharani kwa wawakilishi wetu kimataifa kwa upande wa Wanawake katika Kombe la Dunia.

    Hatua ya kwanza waliweza kuipiga ilikuwa ni kuweza kufuzu na kushiriki Kombe la Dunia kwa timu ya Wanawake ya Tanzania, U 17, Serengeti Girls katika hilo kila Mtanzania alitoa pongezi.

    Kwa sasa ni muda wao wa kuweza kuanza kujipanga upya kwa hatua inayofuata ambayo ni ngumu kuliko ile iliyopita na ilikuwa inasubiriwa kwa shauku kubwa.

    Ikumbukwe kwamba tiketi ya kuweza kuwa hapa ambapo wapo kwa sasa haikupatikana kwa wepesi bali kujitoa na kupambana kwa hali na mali.

    Kupata ushindi wa jumla ya mabao 5-1 mbele ya Cameroon haikuwa jambo jepesi kwani ilionekana jasho la wachezaji hawa lilimwagika huku mbinu za benchi la ufundi nazo zikijibu na kuweza kututoa kimasomaso.

    Sasa U 17 wapo kundi D wanajua kwamba hakuna wepesi kwenye msako wa ushindi na tunaamini kwamba kazi itakuwa nzito katika kila hatua.

    Kutoka kwa ukanda wa Afrika Mashariki Tanzania itakuwa inapeperusha Bendera na inakutana na timu kutoka  Japan,Canada na Ufaransa.

    Kwa walipoweza kufika wanapaswa kuongeza juhudi zaidi kuweza kupeperusha bendera ya Tanzania na Afrika kiujumla katika upande wa soka la Wanawake.

    Ukweli ni kwamba kila timu ambayo imeweza kupenya hapa ni kubwa na ni imara hivyo maandalizi na yaanze sasa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi nzuri huko India.

    Imeandikwa na Dizo Click.

    Previous articleWAKATI MWINGINE KUPIGA HESABU KIMATAIFA
    Next articleYANGA Wafunga BARABARA, MSAFARA Wao HAUJAWAHI KUTOKEA, ANAIMBWA GSM tu HUKO, AZIZ KI Atajwa!