BUGATTI LA RONALDO LAPATA AJALI

MOJA ya magari mawili ya kifahari ambayo, Cristiano Ronaldo alikuwa ameyasafirishwa kwenda Mallorca nchini Hispania kwa ajili ya likizo ya familia yake majira ya kiangazi aina ya Bugatti Veyron limehusika katika ajali baada ya kugonga ukuta nchini Hispania.

Gari hilo ambalo lina thamani ya pauni milioni 1.7 linadaiwa kupata ajali asubuhi ya kuamkia jana katika eneo ya pwani ya mashariki mwa Sa Coma ambapo kwa wakati huo lilikuwa likiendeshwa na mfanyakazi wa mwanasoka huyo, huku Polisi wakiwa wanachunguza tukio hilo lakini bado hawajatoa taarifa rasmi.

Cristiano alisafiri kwenda Mallorca na watoto wake watano na mpenzi wake Georgina Rodriguez mnamo Juni 14, mwaka huu, ambapo wamekodisha nyumba ya kifahari chini ya Milima ya Tramuntana. Pamoja na Bugatti yake Cristiano pia alisafirisha Mercedes-Benz G-Class kwa ajili ya matumizi ya likizo hiyo ya kiangazi.

Mapumziko haya mapya ni ya kwanza kwa wanandoa hao tangu walipotangaza kifo cha pacha wa Esmeralda mnamo Aprili 18, mwaka huu.