SEPP Blatter na Michel Platin ni majina makubwa katika soka ambao kwa pamoja leo wanaingia mahakamani kuendelea kujibu mashtaka ya kujihusisha na rushwa enzi za utawala wao.
Blatter na Platin wanashitakiwa kwa kosa la kuhamisha zaidi ya kiasi cha Euro milioni 1.6 mwaka 2011 kinyume na utaratibu kutoka akaunti ya benki ya Blatter kwenda Platin kiasi cha pesa ambacho kinaelezwa kuwa ilikuwa ni malipo ya kazi aliyoifanya Platin ndani ya Chombo kikubwa cha kusimamia mpira wa miguu duniani FIFA.
Ikumbukwe kipindi hicho Platin alikuwa ni Rais wa Uefa wakati huo Baltter akiwa ni Rais wa FIFA, wote kwa pamoja wamekanusha mashitaka hayo na kudai malipo yalikuwa ni halali kutokana na majukumu ya Platin ndani ya FIFA.
Mnamo mwaka 2015 wawili hao walisimamishwa kujihusisha na soka ambapo Sepp Blatter alifungiwa kujihusisha na soka kwa kipindi cha miaka nane ambapo baadaye ilikuja kupunguzwa hadi kufikia sita na Platin alifungiwa kwa kipindi cha miaka 6 iliyokuja kupunguzwa hadi minne.
Platin raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 66 ni moja ya nguli wa soka duniani na mshindi wa Ballon D’ Or mara tatu na pia alifanikiwa kushinda kombe la mashindano ya Ulaya mwaka 1984 akiwa na timu ya Taifa ya Ufaransa kabla ya kuchukua ubingwa wa Ulaya ngazi ya Klabu mwaka 1985 akiwa na Klabu ya Juventus.
Rufaa yake aliyoikata mwaka 2020 ilikataliwa na Mahakama ya Usuluhishi wa masuala ya michezo CAS.
Kwa upande wake Sepp Blatter ambaye ni raia wa Uswisi mfanyabiashara na kiongozi wa michezo kwa sasa ana umri wa miaka 86 ametumikia kama kiongozi mkuu wa FIFA kwa muda wa miaka 17 ambaye kwa muda wote utawala wake ulikuwa na kashfa nyingi za rushwa, utakatishaji fedha, uhujumu uchumi pamoja na kugushi nyaraka.