TIMU ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 17, Serengeti Girls leo Juni 5,2022 imeweza kukata tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia kwa ushindi wa bao 1-0 Cameroon.
Mchezo wa leo uliochezwa Uwanja wa Amaan,Zanzibar ulikuwa ni wa marudio baada ya ule wa kwanza ugenini Tanzania kushinda mabao 4-1.
Cameroon walikuja leo kwa mpango wa kupindua meza ili waweze kufuzu Kombe la Dunia wakiwa ugenini lakini imeshindikana.
Dakika 45 za mwanzo hakuna timu ambayo iliweza kuona lango la mpinzani mpaka kipindi cha pili ambapo Tanzania waliweza kupata bao pekee la ushindi.
Mtupiaji ni Neema Kinega na kufanya Tanzania kusonga mbele na kufuzu Kombe la Dunia linalotarajiwa kufanyika India kwa jumla ya mabao 5-1.