PABLO ACHIMBA MKWARA WA UBINGWA YANGA

KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco raia wa Hispania, amefichua kuwa anaamini suala la ubingwa kwa Yanga bado gumu kwa kuwa hata wao wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo ikiwa Yanga wataendelea kuangusha pointi katika mechi zao za Ligi Kuu Bara.

Pablo ametoa kauli hiyo kufuatia Yanga kufikisha pointi 57 baada ya mechi 23 wakati Simba ikiwa na pointi 46 baada ya mechi 22. Leo Jumatano Simba wanacheza dhidi ya Kagera Sugar.

Yanga kwa sasa imebakisha mechi saba ambazo sawa na pointi 21 kumaliza ligi wakati Simba ikiwa imebakisha mechi nane sawa na pointi 24.

Akizungumza na Championi Jumatano, Pablo alisema kuwa, suala ya ubingwa kwa wapinzani wao bado gumu kwa kuwa lolote linaweza kutokea kutokana na wao kuendelea kuangusha pointi katika mechi zao wanazocheza hivyo ni suala la wao kuendelea kushinda mechi zao zilizobakia kwenye ligi.

“Nadhani suala la Yanga kuwa ndiyo tayari bingwa siyo kweli kwa kuwa bado ana mechi nyingi ngumu ambazo anapaswa kushinda lakini tayari ameanza kupata matokeo magumu kwenye mechi zao kiasi ambacho kinatufanya tuendelee kuongeza hali ya kupambana kwa kushinda mechi zetu zilizobakia.

“Kikubwa kwetu ni kuongeza nguvu ya kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye mechi zetu zilizobakia kwa kuwa lolote linaweza kutokea ikiwa wataendelea kupata matokeo ambayo wamekuwa nayo kwa sasa,” alisema Pablo.