VILE PUMZI YA MOTO ITAVUTWA LEO UWANJA WA MKAPA

    ILE pumzi ya moto itavutwa kwelikweli kwa wababe wawili wanaotarajiwa kukutana leo Uwanja wa Mkapa,Simba v Ruvu Shooting.

    Ikumbukwe kwamba wababe hawa hawajawa kwenye mwendo unaopendeza hivyo kila mmoja atakuwa anatafuta sehemu ya kutokea na haya yatafanya pumzi ivutwe namna hii:-

    Dakika 270 bila tabasamu

    Wababe hawa wanakutana wakiwa wametoka kukamilisha dk 270 ambazo ni mechi tatu bila tabasamu zaidi ya kuangusha pointi.

    Simba walianza kuangusha pointi mbili mbele ya Polisi Tanzania kisha mbele ya Yanga mechi hizi zote hazikuwa na mabao na kwenye mchezo wa tatu waliambulia sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Namungo FC na kuweza kupunguziwa kasi ya kuufukuzia ubingwa.

    Ruvu Shooting wao walifungana bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania kisha wakapoteza mbele ya Namungo kwa kufungwa mabao 3-1 na mchezo wao uliopita mbele ya Yanga walitoshana nguvu bila kufungana.

    Simba moto utupiaji

    Licha ya kutokuwa kwenye kasi kubwa ya kucheka na nyavu msimu huu Simba bado wamekuwa wamoto mbele ya Ruvu Shooting.

    Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Simba ilishinda mabao 3-1 na jumla kwenye mechi 21 ni mabao 25 Simba imetupia ikiwaacha Ruvu Shooting kwa tofauti ya mabao 6 kwa kuwa wao wana mabao 19 kwenye mechi 21.

    Ulinzi

    Kwa upande wa safu ya ulinzi Ruvu Shooting inaonekana kuwa na tatizo kwenye ulinzi ikiwa imeruhusu mabao 25 kwenye mechi 21.

    Simba ni mabao 9 imetunguliwa katika mechi 21 huku kipa Mohamed Makaka akiwa ameokota nyavuni mabao 20 na Aishi Manula wa Simba katunguliwa mabao 9.

    Hawa wataukosa mchezo

    Mzee wa mguso mmoja, Sadio Kanoute na Hassan Dilunga hawa hawatakuwa sehemu ya mchezo wa Simba kwa kuwa ado hawajawa fiti baada ya kuumiza kwenye mechi za ushindani.

    Kanoute aliumia kwenye mchezo dhidi ya Yanga huku Dilunga yeye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliochezwa Uwanja wa Manungu ukimpa maumivu.

    Ruvu Shooting watakosa huduma ya kiungo wao matata Rashid Juma ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mwisho wa reli Kigoma baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano.

    Msikie Ally

    Ahmed Ally, Meneja wa Idaraja ya Habari na Mawasiliano ndani ya Simba amesema kuwa ile dozi waliyokuwa wakigawa kwenye mashindano ya kimataifa inahamia kwenye ligi.

    “Ile shughuli ambayo tulikuwa tunaoionyesha kwenye mashindano ya kimataifa sasa inahamia kwenye ligi na tuna amini kwamba tutaonyesha kitu cha kipekee,mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,”

    Masau Bwire, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting aliliambia amesema kuwa kwa namna ambavyo wanafanya maandalizi hawana hofu na timu yoyote.

    “Hizi timu zinazodai kwamba ni kubwa sisi hatuna hofu nazo ni muda wetu kuonyesha kwamba tuna uwezo na tutawaonyesha uwanjani,”.

    @Dizo_Click

    Previous articleVIUNGO WA KAZI CHAMA NA SADIO KUIKOSA RUVU SHOOTING
    Next articleSIMBA YATAJWA SARE ZA YANGA