HAWAAMINI macho yao imefika ukingoni kwa mashabiki wa Simba nao kutoamini walichokiona kwa wachezaji wao kushindwa kufikia lengo la kutinga hatua ya nusu fainali.
Kupoteza kwa kufungwa penalti 4-3 mbele ya Orlando Pirates kumezima matarajio ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco kutinga hatua ya nusu fainali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Hesabu zilikuwa ngumu ila kuna jambo la kujifunza kwa wakati ujao kwa wawakilishi wa kimataifa namna hii:-
Matumizi ya uwanja wa nyumbani
Kweli wametolewa lakini wamepata somo lingine kwa namna soka la Afrika lilivyo kwenye matumizi ya uwanja wa nyumbani.
Imeripotiwa kwamba viongozi wa Simba ikiwa ni pamoja na Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez waliweza kuzuiwa mwanzo.
Licha ya uchache wa mashabiki wa Orlando Pirates bado walikuwa na fujo mwanzo mwisho.Hapo kuna jambo wawakilishi wetu kimataifa Simba wanapaswa kujifunza.Kama wangemaliza mchezo Uwanja wa Mkapa kwa kushinda mabao zaidi ya mawili ingekuwa ni habari nyingine.
Manula jezi yake iwekwe makumbusho
Hamna namna licha ya kufungwa bao moja kwenye mchezo wa juzi, bado Aishi Manula aliweza kutimiza majukumu yake kwa kuliweka lango la Simba salama.
Aliweza kuokoa mashuti manne kati ya matano ambayo yalilenga langoni huku moja likiweza kuzama mazima kwenye nyavu zake ilikuwa kupitia kwa Kwame Peprah dk ya 60 kwa kichwa.
Kwenye mikwaju ya penalti, Manula hakuwa na chaguo zaidi ya kuishia kuokoa penalti moja lakini aliweza kutimiza majukumu yake na alionyeshwa kadi moja ya njano katika dk 90 ambazo aliyeyusha.
Hakuna shuti lililolenga lango
Mbinu kubwa ya Simba ilikuwa ni kujilinda jamo lililofanya muziki utumie mabeki kwa asilimia kubwa ikiwa ni pamoja na Henock Inonga, Pascal Wawa,Joash Onyango,Shomary Kapombe,Israel Mwenda na Mohamed Hussein.
Ubunifu eneo la kiungo ulikosekana na mshambuliaji aliyeanza Chris Mugalu aliendelea na makosa kama mechi iliyopita Uwanja wa Mkapa kwa kucheza faulo mwisho alionyeshwa kadi mbili za njano na kutolewa kwa kadi nyekundu.
Mpaka anatoka alikuwa hajapiga shuti hata moja ambalo lilikuwa limelenga lango na kuwaacha wachezaji wenzake dk ya 59 wakipambana.
Mipira iliyokufa imewagharimu
Wakiwa pungufu licha ya kufungwa bao moja waliweza kukomaa nalo mpaka mwisho ila kipengele cha mipira iliyokufa, (penalti) kiliwagharimu Simba kwa kuwa bahati haikuwa yao.
Mpigaji wa kwanza, Jonas Mkude pigo lake liliokolewa na kipa kisha Shomari Kapombe aliweza kufunga huku Henock Inonga yeye aligongesha mwamba na kuwapa nguvu wapinzani wao Orlando Pirates.
Ni Meddie Kagere na Mohamed Hussein hawa penalti zao zilizama nyavuni huku Orlando wao wakifunga penalti 4 na kuifungashia virago Simba ambao walipata penalti 3.
VAR kama VAR
Mfumo wa VAR ulikuwa ni pasua kichwa juzi kwa kuwa uliweza kutumika na kuipa ugumu Simba kupenya kwanza kadi ya njano ya pili kwa Mugalu iliweza kuamuriwa kwa VAR kwa kuwa mwamuzi alikuwa hajaona.
Bao walilofungwa Simba ilionekana kwamba ni mtego wa kuotea lakini hakukuwa na mrejeo wa VAR na dakika za lala salama beki wa Simba, Shomari Kapombe alionekana ameugusa mpira akiwa ndani ya 18 ila mwamuzi wa kati hakuenda kuitazama VAR ngoma ikaendelea.
Simba kimataifa wanaishi ulimwengu wao
Wachezaji wa Simba inapofika kwenye hatua ya kimataifa wamekuwa wakiishi kwenye ulimwengu wao wenyewe kutokana na kucheza kwa kujitoa na kufika hatua ya robo fainali katika hilo wanahitaji pongezi.
Tutaonana baadaye
Bado baadaye tunaweza kuona tena Simba ikafanya kazi yake kwenye hatua za kimataifa kwa kuwa bado wanashiriki Kombe la Shirikisho wakiwa hatua ya robo fainali na wapo kwenye ligi wakiwa nafasi ya pili.