MAKOCHA wa Simba na Yanga, kwa sasa wanapigia hesabu mechi zilizopo mbele yao, huku jicho zaidi likitupiwa Aprili 30, mwaka huu kwenye Kariakoo Dabi.
Ni takribani siku 8 zimebaki kabla ya mchezo huo wa Ligi Kuu Bara kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Hapa Spoti Xtra linakuletea baadhi ya nyota wa kazi katika kikosi cha Yanga kinachonolewa na Nasreddine Nabi sambamba na kile cha Simba chini ya Pablo Franco namna walivyofanya ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu.
YANGA SC
Djigui Diarra
Kipa namba moja wa Yanga, ameanza kikosi cha kwanza mechi 15 akisepa na dakika 1,350, ameruhusu mabao 5 na kakusanya clean sheet 10.
Katika mabao aliyoruhusu, hakuna la mkwaju wa penalti, alianza kuruhusu dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Mkapa mtupiaji akiwa ni Shaban Msala.
Dickson Job
Job kama lilivyo jina lake yale yaliyomo yamo, ni mtu wa kazi kwelikweli akiwa amecheza mechi 16 na kutumia dakika 1,509, ana pasi moja ya bao.
Yanick Bangala
Beki wa kazi ngumu na zile nyepsi akiwa ana uwezo wa kupanda na kushuka, ametumia dakika 1,431, ana pasi moja ya bao.
Saidi Ntibazonkiza
Wamanuita ‘Father’ wa Yanga akiwa ni kiungo mwenye uzoefu mkubwa na soka la ushindani, amecheza mechi 12 katupia mabao 6, ana pasi nne za mabao, kayeyusha dakika 1,048.
Feisal Salum
Mechi 16 kacheza ndani ya Yanga akiwa ameyeyusha dakika 1,325, katupia mabao 4 na pasi 3 za mabao, kazi kubwa ni kwenye kutibua mipango ya wapinzani na kutengeneza nafasi.
Fiston Mayele
Namba moja kwa utupiaji akiwa na mabao 11 na pasi 3 za mabao. Kacheza mechi 19 na kusepa na dakika 1,475.
Djuma Shaban
Mechi zake ni 16 na amefunga mabao 3 na pasi 3 za mabao, huku akisepa na dakika 1,437.
SIMBA SC
Aishi Manula
Air Manula kwenye himaya yake kakaa langoni mechi 16, karuhusu mabao 7 akiwa naclean sheet 9, ameyeyusha dakika 1,440.
Mechi yake ya kwanza kuruhusu bao ilikuwa dhidi ya Ruvu Shooting, ni Elias Maguli ndiye alimtungua.
Henock Inonga
Kazi chafu zinaanza hapa kwenye eneo la kati la ulinzi, katika mechi 13 ambazo kacheza, ni dakika 1,055 kayeyusha, huku akiwa sio mtu mzuri ikiwa utamzingua kwa kuwa kutembeza vichwa kwake sio jambo gumu japo sio mchezo wa kiungwana kama alivyofanya mbele ya Coastal Union na kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Sadio Kanoute
Mtaalamu wa mipira mirefu na mguso wake ni mara moja tu. Kiungo huyo amecheza mechi 8 na kusepa na dakika 668. Katupia bao moja kwa kutumia kichwa akiwa ndani ya 18 na bado hajatoa pasi ya bao.
Bernard Morrison
Mzee wa kuchetua katumia dakika 645 na amefunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao akiwapa Meddie Kagere na Mzamiru Yassin, amecheza mechi 11.
Shomari Kapombe
Ili ukuta wa Pablo ukamilike kisawasawa, utamkuta Kapombe mwenye pasi mbili za mabao na kutumia dakika 1,242.
Meddie Kagere
Kwenye upande wa ushambuliaji kifaru hiki kutoka Rwanda ni namba moja na kimetupia mabao 7 na pasi moja ya bao.
Jonas Mkude
Mkongwe mwenye ujuzi mkubwa akiwa yupo kwenye ubora uleule kwa muda wa takribani miaka 10, mpe kazi ya kucheza na mpira lazima utakubali kazi yake akiwa ametoa pasi mbili za mabao.
Yanga imefunga mabao 33 katika mechi 19 za Ligi Kuu Bara msimu huu.
Simba ikiwa imecheza mechi 19, imepoteza mbili.
Yanga ndiyo timu pekee kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ambayo haijapoteza mechi.