NABI AZIPIGIA HESABU POINTI ZA AZAM FC

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amefunguka kuwa, mipango yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo ujao dhidi ya Azam kutokana na kuwa na malengo ya kuchukua ubingwa msimu huu licha ya kuandamwa na wimbi la majeruhi.

Aprili 6, mwaka huu, Yanga inatarajiwa kucheza dhidi ya Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar.

Yanga inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 48, ikifuatiwa na Simba wenye 37, wakati Azam wana 28.

 Nabi amesema: “Tunahitaji kuona timu inapata ushindi kwa sababu tunaelewa haitokuwa mechi nyepesi kwetu kutokana na wapinzani kuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.

“Lakini jambo ambalo tunaweza kuliangalia ni jinsi ya kupata matokeo bora katika mchezo huo ili kufikia malengo ya ubingwa kwa kuongeza idadi ya pointi.

“Sisi hatuna presha licha ya kuwa huenda baadhi ya wachezaji kama Khalid Aucho kutokuwepo kutokana na majeraha aliyopata, lakini jambo ambalo tunaweza kuliangalia kwa upande wetu ni kupata matokeo mazuri na kufikia malengo ambayo tumejiwekea.”

Chanzo:Spoti Xtra