Home Sports MTAMBO WA MABAO YANGA HATIHATI KUIKOSA AZAM

MTAMBO WA MABAO YANGA HATIHATI KUIKOSA AZAM

IMEFAHAMIKA kuwa, kiungo tegemeo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amepata majeraha yaliyomfanya aondolewe kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, hivyo kuna uwezekano mkubwa akaikosa mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam itakayochezwa Aprili 6, mwaka huu.

Kwa sasa Taifa Stars ipo kambini kwa ajili ya kucheza mechi za kirafi ki ambapo tayari imecheza dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kushinda 3-1, jana Jumanne ilicheza dhidi ya Sudan na kufungana bao 1-1.

Daktari Mkuu wa Viungo wa Yanga, Youssef Ammar, alithibitisha kupata taarifa za Fei Toto kupata majeraha akisema: “Nimepata taarifa za Fei Toto kupata majeraha akiwa na timu ya taifa. Lakini nisingependa kulizungumzia hilo kwa hivi sasa kwani ninamsubiria mara baada ya kurejea kambini Yanga nitajua nini tatizo baada ya kupata ripoti ya daktari wa timu ya taifa.

Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen, alizungumzia majeraha ya Fei Toto akisema: “Feisal tumemtoa kwa sababu amepata majeraha.”

Mwakilishi kutoka Idara ya Tiba ya Taifa Stars, alisema Fei Toto aliumia tangu Januari 26, mwaka huu akiwa na kikosi cha Yanga.

“Vipimo vilifanyika na ikaonesha Feisal amepata majeraha ambayo ni makubwa kwani msuli mdogo umechanika.

“Tunaona wakati ule alipoumia hakupata matibabu ya kutosha, alipokuja kwetu tukamuangalia tukagundua hilo, tungeweza kumtumia, lakini tungefanya maisha yake ya soka kuwa mafupi, tumemruhusu ili apate matibabu sahihi.”

Fei Toto ni mtambo wa mabao namba tatu katika kikosi cha Yanga msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara akihusika kwenye mabao saba baada ya kufunga manne na asisti tatu, nyuma ya Saidi Ntibazonkiza (mabao 6, asisti 4) na Fiston Mayele (mabao 10, asisti 3 )

Chanzo:Spoti Xtra

Previous articleMUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATANO
Next articleGHANA YAFUNZU KOMBE LA DUNIA,VURUGU KUBWA YATOKEA