LICHA ya staa mkubwa wa Hollywood, Will Smith kuomba msamaha jukwaani baada ya kumzaba kofi mchekeshaji Chris Rock, staa huyo pia ametumia akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa Instagram kuendelea kuomba radhi, safari hii akimuomba pia radhi Rock kwa kitendo alichomfanyia.
Will Smith ameandika:“Vurugu katika namna yake yoyote ni sumu na hubomoa. Tabia yangu usiku uliopita katika tukio la utoaji wa tuzo haikubaliki na haisameheki.
“Utani kuhusu mimi ni sehemu ya kazi yangu lakini utani kuhusu ugonjwa wa mke wangu ulivuka mipaka na kunifanya nishindwe kudhibiti hisia zangu.
“Napenda kuomba radhi hadharani kwako Chris. Nilitoka nje ya mstari na nilikosea. Najisikia vibaya kwamba tukio hilo limeenda tofauti na mipango ya jinsi ninavyotaka kuwa.
“Hakuna nafasi ya vurugu katika dunia iliyojawa upendo na huruma,” aliandika Smith.
Pia ameomba radhi kwa mara nyingine kwa waandaaji wa tuzo hizo na familia ya Williams ambayo kupitia filamu waliyoitengeneza kuhusu maisha yao, ndiyo Smith aliyopatia tuzo.
Bado Rock hajajibu chochote kuhusu msamaha huo wala hajatoa maoni yoyote lakini wanaharakati mbalimbali wanaendelea kupaza sauti wakitaka staa huyo anyang’anywe tuzo hiyo kwa kuonesha tabia mbovu hadharani.