KUSHINDWA kupata matokeo kwenye mechi moja ugenini haina maana kwamba kazi imekwishwa na hakuna uwezo wa kupata ushindi kwa mechi zijazo hapana.
Ipo wazi kwamba ilikuwa kazi kubwa kusaka pointi ugenini mwisho wa siku wawakilishi wetu kwenye mashindano ya kimataifa wakapata pointi moja kati ya sita ambazo walikuwa wanazisaka.
Makosa yapo na nina amini kwamba benchi la ufundi limeona wapi ambapo walikosea na wanajua kwa nini walipata hicho ambacho wamekipata.
Ukweli ni kwamba kwa sasa Watanzania wanapenda kuona timu inapata matokeo mazuri na kusonga mbele mpaka hatua ya robo fainali lakini haitawezekana ikiwa wachezaji hawatatimiza majukumu yao.
Naongea na mashabiki wa Tanzania kiujumla wazidi kuwa pamoja na Simba katika mashindano ya kimataifa ili waweze kufanya vizuri.
Ushindi kwa mchezo wa kwanza nyumbani na sare huenda iliwapa amani kwamba wanaweza kushinda mbele ya RS Berkane lakini mambo yalikuwa tofauti.
Kwenye ulimwengu wa mpira tunasema kwamba makosa yanaigharimu timu hivyo mpaka sasa Simba imefanya makosa manne kwenye mechi za kimataifa jambo linalofanya waweze kufungwa mabao manne kwenye mechi tatu.
Kuna jambo la kufanya kwenye safu ya ulinzi ikiwa imeweza kufungwa kwenye mechi zote za kimataifa hapo ni lazima benchi la ufundi kuweza kujua nini kifanyike ili mechi zijazo matokeo yapatikane.
Kila mchezaji anapenda kutimiza majukumu yake na kila mchezaji anapenda furaha hivyo furaha iwe kila mechi kutimiza majukumu bila kukata tamaa.
Ukija kwenye safu ya ushambuliaji pia benchi la ufundi nina amini kwamba linatambua suala hilo muhimu kuweza kufanya kazi kwa mara nyingine kuweza kufanya maboresho zaidi na zaidi.
Ikiwa wachezaji watafikiria kazi imekwisha kwa hatua ambayo wamepiga na pointi moja waliyopata ugenini kuna jambo linaweza kuwakuta kwenye mechi ambazo watacheza Uwanja wa Mkapa.
Katika mechi za msako wa pointi tatu kimataifa ni hesabu tu huwa zinacheza yule ambaye atachanga vema karata yake basi ushindi unakuwa mikononi mwake.
Mbinu zikiwa ni zilezile basi hakutakuwa na muda wa kuweza kupata matokeo mazuri hivyo tunaamini kwamba makosa ambayo yametokea yatafanyiwa kazi.
Kwa mashabiki ni muda wa kuendelea kuzishangilia timu zao kwenye mechi za kimataifa pamoja na mashindano ambayo yanaendelea kwa wakati huu.
Napenda kuzikumbusha timu kwamba kwa sasa ni mzunguko wa pili hivyo na mbinu zinapaswa kubadilika na hesabu kuwa tofauti kwenye kila mchezo ili kupata pointi tatu.
RS Berkane ni timu imara lakini inafungika ikiwa kutakuwa na mipango makini na mashabiki pia wazidi kujitokeza uwanjani kushangilia timu zao.
Yote yanawezekana ikiwa kutakuwa na maandalizi mazuri kila hatua na kufanya kazi bila kukata tamaa.