SIMBA YATUMIA MBINU YA KIPEKEE KUIMALIZA RS BERKANE

KATIKA kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo wao wa kesho Jumapili dhidi ya RS Berkane, uongozi wa Simba umeamua kutumia njia ya kipekee kupitia uhusiano wao na maofisa wa Raja Casablanca ya Morocco kuhakikisha wanapata mbinu za kuwamaliza Berkane.

Simba inanufaika kutokana na kuwa na makubaliano ya ushirika na Klabu ya Raja Casablanca yaliyotokana na ziara ambayo aliifanya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez mwaka jana katika nchi za Morocco na Misri.

Akizungumzia mapokezi yao kutoka kwa uongozi wa Raja Casablanca ya Morocco baada ya kuwasili nchini humo, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema:“Tunashukuru kwa kufanikiwa kufika salama hapa Morocco baada ya safari ndefu kutokea nchini Uturuki, ambapo tulikuwa na mapumziko ya muda mfupi baada ya kutokea nchini Niger.

“Jambo lililotufurahisha zaidi ni mapokezi mazuri ambayo tumeyapata kutoka kwa uongozi wa Klabu ya Raja Casablanca ya hapa ambao kwa kiasi kikubwa wameshirikiana na viongozi wetu waliotangulia hapa kuhakikisha tunafikia mahali salama na pia kupeana uzoefu juu ya wapinzani wetu na kuhakikisha tunafanya vizuri.”

Simba ikiwa Morocco ilitumia pia basi kubwa la Raja Casablanca shuhuli zake nchini humo na leo imewasili salama mji wa Berkane kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wa kesho.