UONGOZI wa Klabu ya Simba, umetoa onyo kali kuwa wapinzani wao wasifikiri ratiba ya mashindano ya kimataifa itawapotezea hesabu walizonazo kwenye Ligi Kuu Bara.
Simba kwa sasa ipo bize na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa Kundi D, ambapo wikiendi hii itacheza dhidi ya RS Berkane nchini Morocco.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba ipo nafasi ya pili na pointi zao 31 walizokusanya kwenye michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema: “Ni kweli tuna kazi ngumu na muhimu sana ya uwakilishi kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hii haimaanishi tumesahau kabisa au tutabweteka na mipango tuliyonayo kwenye michuano ya ndani hususani Ligi Kuu Bara.
“Tuliamua kusafiri na kundi kubwa la wachezaji kwa sababu tunataka kuhakikisha maandalizi tunayofanya yatusaidie kufika mbali kwenye michuano ya Afrika, na kutumia uzoefu huo kuzidi kupata matokeo mazuri tutakaporejea kwenye Ligi Kuu, hivyo wapinzani wetu wajiandae.”