SIMBA MNA KAZI YA KUFANYA KIMATAIFA,ISHU YA MASHABIKI IFANYIWE KAZI

    HATUA kubwa ambayo mmefanya kwa ushindi kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Mkapa mnastahili pongezi wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho.

    Simba hamjafanya jambo dogo kwa kushinda mabao 3-1 dhidi ya ASEC Mimosas Uwanja wa Mkapa hakika mnastahili pongezi lakini ukweli ni kwamba kazi ndiyo kwanza inaanza.

    Vigongo ambavyo vinakuja kwenu ni vikubwa na ushindani ni mkubwa mkishindwa kufanya vizuri mtapoteana na kwenye ligi pia kama ambavyo mlianza msimu kwa kusuasua.

    Ukweli ni kwamba mechi za kimataidfa zinahitaji akili kubwa katika kuzimaliza na kupata matokeo kwa kuwa ni mwendo wa msako wa pointi tatu muhimu na kushinda mechi za mwanzo kunaongeza hali ya kujiamini.

    Hakuna ambaye alikuwa anatarajia kuona mchezo mwepesi mbele ya ASEC Mimosas kwa kuwa ni mchezo ambao ulikuwa na ugumu kwa pande zote mbili.

    Lakini mbali na ushindi bado kuna makosa ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi hasa katika kutengeneza nafasi na kuzimaliza hasa ndani ya 18.

    Matumizi ya mapigo huru hasa kona kwa sasa imekuwa ngumu Simba kimataifa kushinda kwa mabao hayo na ni rahisi Simba kufungwa aina hiyo ya mabao.

    Kumbuka mchezo ulioiondoa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa dhidi ya Jwaneng Galaxy ilikuwa ni mwendo wa mapigo huru kwa asilimia kubwa yaliipa tabu safu ya ulinzi ya Simba nina amini kwamba makosa hayo yatafanyiwa kazi.

    Ajabu kubwa ambayo nimeiona Uwanja wa Mkapa sikutarajia kuona hasa kwa mashabiki wa Simba kuonekana wakiwafanyia fujo mashabiki ambao walikuwa wakionekana kuwa ni wa Yanga kutokana na jezi ambazo walikuwa wamevaa.

    Hii akili inatoka wapi tena kwenye ardhi ya Tanzania hili jambo ni baya sana halipaswi kupewa kipaumbele na kurudiwa tena.

    Ajabu ya pili ni namna Simba walivyochukulia jambo hili kwa wepesi kwamba mashabiki waliojitokeza hawapati burudani sehemu waliyopo, kweli kabisa taarifa inayohusu maisha ya watu unataja burudani?

    Ngumu sana kuamini lakini ukweli ni kwamba wale mashabiki wanapenda mpira na walitoa fedha zao na muda kwa ajili ya kuona burudani suala la kushangilia timu ipi hilo linawahusu mashabiki kwa sababu kuna wakati mashabiki wa Simba wanavaa jezi zao lakini hawaishangilii Simba.

    Mpira sio ugomvi, mpira sio lazima kila mmoja ashangilie ndio maana mashabiki wote wanaojitokeza uwanjani wapo ambao wanamaliza dakika 90 bila hata kushangilia,kila mtu kuna anachokipenda.

    Yupo shabiki furaha yake ni kumuona mchezaji fulani akiwa uwanjani hapo anakuwa amemaliza kile anachokifuata suala la kushangilia anawaachia wengine, basi kwa kuwa imetokea ni lazima ikemewe upya na taarifa pia itolewe upya na sio kishkaji hapana haileti maana.

    Maisha ya watu huwezi kuweka utani wa jadi ni lazima ichukuliwe kwa uzito mkubwa nina amini kwamba mashabiki wataendelea kuwa pamoja na kushirikiana.

    Kwa mechi zijazo Simba msisahau kwamba mmebeba furaha ya Watanzania,makosa ambayo mmeyafanya nina amini kwamba benchi la ufundi limeona na litafanyia kazi.

    Na hili la mashabiki viongozi nina amini kwamba mtazungumza upya inaweza ikatokea mkazuiwa fursa ya mashabiki kuingia uwanjani kisa kidogo ambacho mnaita burudani.

    Pia kwa mechi yenu ambayo inatarajiwa kuchezwa kesho dhidi ya USGN ya Niger tunaamini kwamba itakuwa ni kazi kwenu kuipeperusha bendera ya Tanzania.

    Kila la kheri Simba na maombi yetu ni kuona kwamba mnapata matokeo chanya kwenye mechi hiyo muhimu na mchezo wenu wa tatu pia mbele ya RS Berkane imani yetu ni kuona kwamba mnashinda.

    Previous articleKOCHA AFUKUZWA,MRITHI WAKE KUANZA KAZI LEO
    Next articleMSHAMBULIAJI WA SIMBA RUKSA KUIVAA YANGA