MSHAMBULIAJI WA SIMBA RUKSA KUIVAA YANGA

MTIBWA Sugar imethibitisha kuwa muda wowote kuanzia sasa, itaanza kumtumia winga wao raia wa DR Congo, Deo Kanda baada ya kila kitu kukamilika.

Thobias Kifaru,Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar amesema kuwa walikuwa wanashindwa kumtumia nyota huyo kwa sababu kuna vitu kuhusu uhamisho wake vilikuwa havijakamilika ila kwa sasa kila kitu kipo sawa.

Ikumbukwe kwamba nyota huyo aliwahi kucheza ndani ya kikosi cha Simba na aliwahi kuwafunga Yanga kwenye mchezo wa ligi walipokutana Uwanja wa Mkapa.

  Kifaru amesema: “Tunatarajia kuanza kumtumia Deo Kanda hivi karibuni changamoto ilikuwa upande wa wenzetu kushindwa kutuma kibali chake.

“Deo Kanda tulimsajili sisi wakati wa dirisha dogo ila hakuwa anaonekana uwanjani kwa sababu ya kibali chake lakini mawasiliano yamefanyika tayari na wenzetu.

“Na tutakipata hivi karibuni, yeye mwenyewe anatamani kuitumikia Mtibwa Sukari. Kama itakuwa sawa huenda akacheza dhidi ya Yanga.”

Kanda aliibuliwa na Motema Pemba ya DR Congo, kisha akajiunga na TP Mazembe, Vita Club, Raja Raja Casablanca, Simba na nyingine.