MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, ametamba kuwa, malengo waliyojiwekea msimu huu ni kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo kwa kuanza wataanza kuchukua pointi tatu mbele ya ASEC Mimosas, kisha RS Berkane.
Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Saalaam, Simba itapambana na ASEC Mimosas, ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambapo timu hizo zipo Kundi D.
Msimu uliopita, Simba iliishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku malengo yakiwa ni kufika nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mangungu alisema kikubwa walichopanga msimu huu ni kuvuna pointi tatu katika kila mchezo watakaocheza nyumbani kwenye Uwanja wa Mkapa.
Aliongeza kuwa, hakuna kitakachoshindikana kwao kutokana na maandalizi makubwa waliyoyafanya chini ya Kocha Mkuu, Pablo Franco raia wa Hispania.
“Niwaombe mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi Jumapili hii katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya ASEC Mimosas utakaochezwa Uwanja wa Mkapa.
“Uwepo wa mashabijki uwanjani ndiyo chachu ya ushindi katika mchezo huo ambao muhimu kupata pointi tatu katika uwanja wetu wa nyumbani.
“Simba imekuwa na historia ya kipee katika michuano ya kimataifa tangu miaka ya 1970, kama uongozi tumeshakamilisha maandalizi yote ya mchezo huo,” alisema Mangungu.