SIMBA YATAJA NAMNA ITAKAVYOTWAA UBINGWA WA LIGI

PABLO Franco, Kocha Mkuu wa Simba ameweka wazi kuwa mbinu pekee ya timu hiyo kutwaa ubingwa msimu huu na kuwafunika wapinzani wao Yanga ni kushinda mechi ambazo watacheza.

Simba ni mabingwa watetezi, wanapambana kufikia malengo yao wakiwa wamejichimbia nafasi ya pili na pointi 28 huku wakiwa wamepoteza mechi mbili kati ya 14.

 Pablo amesema kuwa hana mashaka na wachezaji wa kikosi cha Simba kwa namna wanavyocheza licha ya kushindwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi walicheza ugenini hivi karibuni.

“Bado malengo yetu ni kutwaa ubingwa kwani inawezekana na hilo lipo kwetu sisi. Jambo pekee ambalo litatupa nafasi ya kutwaa ubingwa ni kushinda mechi zetu ambazo tutacheza na hilo lipo wazi.

“Ninafurahishwa na kazi ambayo inafanywa na wachezaji uwanjani licha ya kushindwa kutumia nafasi ambazo tunazipata, hilo ni jambo ambalo tunapaswa kulifanyia kazi,” amesema Pablo.

Mchezo ujao wa Simba kwenye ligi ni dhidi ya Mbeya Kwanza unatarajiwa kuchezwa leo Jumapili.

Ikumbukwe kwamba kwenye mechi tatu za ugenini Simba kwenye msako wa pointi 9 ilisepa na pointi moja pekee na safu yake ya ushambuliaji haikufunga bao hata moja.