TANZANITE WAREJEA DAR SALAMA WAKITOKEA ETHIOPIA

TIMU ya taifa ya Wanawake chini ya miaka 20, Tanzanite Queens leo Februari 5 imerejea salama Tanzania ikitokea nchini Ethiopia ambapo ilikuwa na kazi ya kuipeperusha bendera  kwenye mashindano ya kimataifa.

Jana ilikuwa kwenye mchezo wa pili dhidi ya Ethiopia baada ya ule wa awali uliochezwa Uwanja wa Amaan ubao kusoma Tanzanite 1-0 Ethiopia na ilikuwa inahitajika sare ama ushindi kuweza kusonga mbele.

Baada ya dakika 90 ubao ulisoma Ethiopia 2-0 Tanzanite na kufanya Tanzanite kuondolewa kwa jumla ya mabao 2-1 hivyo leo wamerudi kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mashindano mengine.

Bakari Shime, Kocha Mkuu wa Tanzanite amesema kuwa wameumizwa na matokeo hayo kwa kuwa walipata nafasi nyingi ila wakashindwa kuzitumia jana.

“Tulipata nafasi lakini tulishindwa kupata matokeo na mwisho wa siku tumetolewa haya ni maumivu lakini ni mpira kwa kilichotokea tunajipanga upya kwa ajili ya mashindano mengine,”.

Wilfred Kidao, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) amesema kuwa wamepokea matokeo hayo kwa maumivu lakini hakuna namna kwenye mashindano hayo yanatokea.

“Tulikuwa tunahitaji ushindi na hilo wameonyesha vijana wetu wamepambana ila wamekosa matokeo hivyo tunajipanga kwa ajili ya mashindano mengine ambayo yanakuja kwa walichokifanya mabinti wetu wanahitaji pongezi,”.