CHEKI DAKIKA 360 ZA MOTO YANGA FEBRUARI

NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga kwa sasa ana dakika 360 za moto kusaka ushindi kwenye mechi za ushindani zinazotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ndani ya Februari.

Ikiwa inaongoza ligi na pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 13 inakigongo cha moto Februari 5, Uwanja wa Mkapa itakuwa dhidi ya Mbeya City.

Mbeya City imekuwa kwenye mwendo bora ikiwa nafasi ya 3 na pointi zake 22 imepoteza mchezo mmoja pekee ilikuwa ugenini dhidi ya Coastal Union kwa kufungwa mabao 3-2 na ni timu ya kwanza kuitungua Simba ndani ya ligi msimu wa 2021/22.

Baada ya kukamilisha mchezo huo Nabi atakuwa na kibarua kati ya Februari 12/17 kumenyana na Biashara United huu utakuwa ni mchezo wa hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Shirikisho.

Kituo kinachofuata itakuwa ni Februari 23 pale Uwanja wa Manungu dhidi ya Mtibwa Sugar.

Mbele ya Kagera Sugar itakuwa ni Februari 27 Uwanja wa Mkapa itakuwa ni kete itakayokamilisha safari ya dakika 360 za kusaka ushindi ndani ya mwezi huu.

Nabi amesema kuwa kazi kubwa iliyopo kwenye mechi zao zote ni kusaka ushindi bila kujali wanacheza na timu ipi.