AZAM FC WANAUTAKA UBINGWA WA KOMBE LA FA

KOCHA Mkuu wa Azam raia wa Marekani,  Abdi Hamid Moallin ameweka wazi kuwa kipaumbele chake kikubwa
mara baada ya kurasimishwa kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, ni kuhakikisha wanashinda ubingwa wa
Kombe la Shirikisho la Azam (FA) linalotetewa na Simba.

Moallin alitangazwa rasmi kuchukua majukumu ya ukocha mkuu ndani ya kikosi chaAzam
Januari 25, mwaka huu mara baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa mafanikio kama kaimu kocha mkuu tangu Desemba mwaka jana.

Tayari chini yake Azam kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam wamefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora mara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa hatua ya 32 bora dhidi ya Transit Camp, ambapo sasa watavaana na Baga Friends.

Kocha Moallin amesema: “Ni jambo zuri kuona kikosi chetu kimefanikiwa kufika hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho, tunayo malengo mengi kama timu msimu huu.

“Lakini lengo kubwa la muda mfupi ni kuhakikisha tunapata nafasi ya kucheza fainali ya michuano hii na kutwaa ubingwa, ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kucheza mashindano ya kimataifa mwakani.”