ISHU YA KUBEBA MATOKEO MFUKONI IWEKWE KANDO

KILA mmoja kwa sasa kwenye ligi anavuna kile ambacho alikipanda wakati wa maandalizi na hakuna bahati mbaya ambayo inatokea.

Ikumbukwe kwamba ni muda mfupi tumetoka kukamilisha dirisha dogo la usajili ambalo lilikuwa lina mambo mengi na sarakasi za kutosha mwisho wa siku kila kitu kimekuwa wazi.

Ilikuwa namna hiyo kwa wale ambao walikuwa wanahitaji kufanya hivyo wamekamilisha hesabu zao na kuna timu nyingine ziliweka wazi kwamba hazina mpango wa kuongeza nguvu kwa kuwa wanajitosheleza hilo nalo ni sawa.

Wapo ambao walifanya kwa mujibu wa mashabiki na sio benchi la ufundi na wapo ambao walifanya kwa mujibu wa benchi la ufundi yote maisha na hili ni soka letu linakwenda kwa mtindo wake.

Kila timu kuanzia Championship, Ligi Kuu Bara mpaka Ligi ya Wanawake walikuwa na muda wa kufanya maboresho na ikiwa walikwama basi ni wakati mwingine kutazama pale ambapo walishindwa kisha wakatibu tatizo kwa wachezaji walewale walionao.

Licha ya usajili ambao umefanyika bado ukweli ni kwamba hakuna mchezaji,shabiki ama kiongozi anayepaswa kwenda uwanjani na matokeo.

Suala la kubeba matokeo hakuna bali dakika 90 hizo zinatosha kuamua matokeo yanayotakiwa.

Wale ambao wapo Ligi Championship wanajua  namna ushindani ulivyo mkubwa na kila timu inavyopambana kusaka ushindi kwenye mechi zake huku kila mechi ni fainali.

Hamna namna ya kufanya kwa sasa kwa kuwa maisha lazima yaendelee na kwa kuwa kwenye ushindani ni lazima aonekane ambaye anashindwa.

Zipo ambazo zimekuwa zikishindwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi zao ambazo zimepita hilo ikiwa halitafanyiwa maboresho kwa sasa litaendelea tena kwa mara nyingine tena.

Kwa wachezaji ambao wamepata timu mpya kwa wakati huu na wale ambao wameongeza mikataba yao basi wajue kwamba kazi yao ni moja kucheza mpira.

Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi itaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.

Kasumba ya timu nyingi kuonyesha ushindani mzunguko wa pili isipewe nafasi na badala yake kila mmoja kwa sasa apambane kufanya kweli kwenye mechi zote na inawezekana.

Ushindani na ule mchezo wa kusaka pointi tatu ni muhimu uwe unaonekana kwenye kila mechi bila kujali ni timu ipi ipo nafasi ipi.

Kila kitu kinawezekana ikiwa kutakuwa na mpango makini na ukweli ni kwamba kupanda ni rahisi na kushuka ni rahisi pia lakini ukishashuka kurudi huku juu huwa inakuwa ngumu.

Wachezaji wakiweza kufanya yale ambayo wanaelekezwa na benchi la ufundi inakuwa ni rahisi kwao kupata ushindi pia jitihada binafsi zinahitajika kwa wachezaji katika kusaka matokeo.

 Zipo timu ambazo ziliwahi kupanda daraja  zilianza vizuri mwanzo lakini zilipokuja kukwama kusaka matokeo ziliweza kurejea zilikokuwa zimetoka hili nalo liwe ni somo kwa timu zote.

Matumaini yangu ni kwamba kupitia matukio haya yanayoendelea wamiliki wa timu, wachezaji pamoja na wamiliki wa timu wanaona namna mambo yanavyokwenda hivyo wataongeza umakini wakati watakapokuwa kwenye ushindani.

Tunataka kuona timu ikipanda kwenye ligi iwe na uwezo na vigezo vya kuhimili mikikimikiki ya huku kwani hakuna kuzubaa ni mwendo wa kukimbizana.

Kila timu ambayo ipo chini inahitaji kuja juu hilo lipo wazi hivyo kikubwa ni kuona kwamba kila timu inapata ushindi na kufanya vizuri.

Uzuri ni kwamba mchezo wa mpira ni mchezo wa wazi yule ambaye atakwama kwenye mbinu basi hakuna namna atapoteza tu.

Jambo la msingi kwa sasa kila mchezaji kujua wajibu wake na kutimiza majukumu yake kwa umakini ili ushindi upatikane wa ajili ya timu.

Mashabiki pia mnapaswa muelewe kwamba suala la kwenda uwanjani na matokeo halina nafasi, mpira dakika 90 hapo nani atajulikana amepata nini.

ReplyForward