MKUDE AFUNGA 2021 NA REKODI HII

JONAS Mkude, kiungo wa kazi zote chafu ndani ya uwanja amefunga kibabe mwaka 2021 kwa kutoa pasi yake ya kwanza ambayo ilikuwa ni zawadi ya Krismasi kwa mashabiki wake.

Kiungo huyo ambaye kwa sasa ni chaguo la kwanza chini ya Kocha Mkuu, Pablo Franco awali zama za Didier Gomes hakuwa na nafasi ya kucheza kutokana na suala la utovu wa nidhamu.

Ndani ya ligi amecheza jumla ya mechi sita na kuyeyusha jumla ya dakika 496 na pasi yake ya kwanza alitoa Desemba 24 kwenye mchezo wa ligi dhidi ya KMC.

Ilikuwa ni dakika ya 10, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi alimpa mshikaji wake Mohamed Hussein aliyemtungua bao la kwanza Faroukh Shikalo kipa wa KMC ambaye aliokota jumla ya mabao manne kwenye mchezo huo.

Pia mbali na Mkude kutoa pasi yake ya kwanza hata nahodha msaidizi Mohamed naye alifunga bao lake la kwanza kwa msimu wa 2021/22.

Kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 9 Simba imefunga mabao 12 ipo nafasi ya pili na pointi zake 21 kinara ni Yanga mwenye pointi 26 baada ya kucheza mechi 10.