KOCHA Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi amesema kuwa hana hofu kukosekana kwa beki wake wa pembeni, Shomari Kibwana kwani tayari yupo mbadala wake David Bryson anayemuandaa kuchukua nafasi yake.
Kibwana anatarajia kukaa nje ya uwanja kwa wiki nne akiuguza majeraha ya goti aliyoyapata katika mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Simba wikiendi iliyopita uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo wapo wachezaji wawili anaowandaa watakaochukua nafasi ya Kibwana ambao ni Bryson na Yassin Mustapha.
“Nabi anavutiwa na aina yake ya uchezaji hasa katika kuanzisha mashambulizi kutokea pembeni na kulinda golini kwake.
“Kwa muda mrefu alikuwa akimuandaa katika michezo ya ligi kwa kutokea benchi akichukua nafasi ya Kibwana katika kipindi cha pili.
“Hivyo katika mchezo wa kesho (Jumapili) Bryson ataanza moja kwa moja katika kikosi cha kwanza na Yassin akiwa benchi,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo, Nabi alisema: “Bryson ni mchezaji mzuri amekuwa akikosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza kutokana na changamoto ya ushindani aliyoikuta katika timu.
“Kwani tayari alikuwepo Kibwana aliyekuwepo katika kiwango bora katika msimu uliopita, ngumu kumtoa na kumuingiza yeye kwa haraka kutokana na uaminifu niliokuwa nao kwake,” alisema .