>

MZEE WA KUCHETUA BM APIGWA ‘STOP’SIMBA

MZEE wa kuchetua ndani ya kikosi cha Simba, Bernard Morrison amepigwa ‘stop’ kucheza faulo za akiwa kwenye mazoezi kwa wachezaji wengine ili kuepusha maumivu yasiyokuwa na lazima.

Novemba 16 kwenye mazoezi ya Simba yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veteran, Morrison alikuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa kwenye mazoezi hayo chini ya Kocha Mkuu, Pablo Franco, wasaidizi Seleman Matola, Hitimana Thiery na kocha mpya wa viungo Don Daniel.

Katika mazoezi hayo Morrison alionekana kumchezea faulo Shomari Kapombe alipokuwa akiwania mpira jambo lililofanya Kapombe kuanguka nje ya uwanja kwa nguvu huku wachezaji wengine wakimshangaa Morrison.

Kutokana na kitendo hicho Kapombe alionekana kupoteza ile furaha ya kuendelea kukabwa na Morrison na Hitimana alipoona hilo alionekana akimwambia Morrison aache kucheza faulo kwa kuwa hazitakiwi kwenye mazoezi.

Morrison alionekana akijibu kwa kusema kuwa alicheza mpira na wala hajacheza faulo na alimfuata Kapombe kumpa mkono ndipo Pablo alipoamua kumfanya Morrison awe upande wa Kapombe kabla ya kuendelea na mazoezi mengine.

Kikosi cha Simba kesho kinatarajiwa kushuka Uwanja wa CCM Kirumba kusaka pointi tatu mbele ya Ruvu Shooting na tayari kimeshawasili Mwanza na Morrison ni miongoni mwa wachezaji ambao wapo kwenye kikosi.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu zote mbili kupiga hesabu ya kusepa na pointi tatu muhimu.