>

YANGA WAANDAA JAMBO KUBWA KWENYE USAJILI

KATIKA kuelekea usajili wa dirisha la Januari, mwaka huu wadhamini wa Yanga, Kampuni ya GSM, wamewahakikishia mashabiki wa timu hiyo kufanya usajili mkubwa na wa kishindo.

 

Yanga imeonekana kudhamiria msimu huu kutwaa mataji yote wanayoshindania ikiwemo Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), ambayo yote yanatetewa na Simba.

 

Timu hiyo tayari imeanza kubeba mataji hayo kwa kuchukua Ngoa ya Jamii waliyoichukua kwa kuwafunga watani wao Simba bao 1-0 mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, Septemba 25.

 Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM na Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, Injinia Hersi Said, amesema kuwa kama wadhamini wamepanga kutumia kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya uwekezaji Yanga.

Said mesema kuwa uwekezaji huo waliopanga kuanza nao ni katika usajili wa wachezaji bora wenye uwezo mkubwa zaidi ya nyota wapya waliowasajili akina Khalid Aucho, Yannick Bangala, Shabani Djuma, Jesus Moloko, Fiston Mayele na Djigui Diarra.

 

Aliongeza kuwa wachezaji wawili wa kigeni ndio waliopanga kuwasajili pekee Januari, lengo ni kufanikisha mahitaji ya kocha aliyoyatoa katika kamati husika.

 

“Usajili bora tulioufanya ndiyo umetufanya kucheza michezo mitano ya ligi bila kufungwa huku tukikaa kileleni katika msimamo wa ligi, siyo kitu kidogo kwetu.

“Ubora huo wa wachezaji ndiyo sababu ya wachezaji wetu kujituma na kila mmoja kuonyesha ushindani na kujituma uwanjani kila anayepata nafasi ya kucheza.

 

“Mfano Yanga ya hivi sasa mchezaji kama Mukoko na Saido wanaanzia benchi ambao msimu uliopita walikuwa tegemeo.

“Hiyo inaonyesha jinsi gani msimu huu tuna timu iliyo bora na kuleta ushindani wa kimataifa na timu yoyote ndani na nje ya nchi.

 

“Kama wadhamini bado hatujaridhika na ubora wa kikosi hicho na badala yake tutaendelea kukiboresha kikosi chetu kwa kusajili wachezaji bora na tishio katika ukanda huu wa Afrika.

“Tunajivunia uwepo wa bosi wetu wa GSM, Ghalib ambaye yeye anataka kuona Yanga inakuwa bora kwa kuhakikisha anafanikisha usajili wa wachezaji wa kiwango kikubwa Afrika,” amesema.