KUMEIBUKA taarifa kuwa Polisi Tanzania wapo kwenye mpango wa kuwasajili viungo wawili wa Azam FC, Mudathir Yahya na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ ambao wamesimamishwa.
Taarifa hizo zinadai kuwa, Polisi Tanzania wanawataka nyota hao ili kuimarisha kikosi chao na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwania nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa ligi mwisho wa msimu.
Chanzo hicho kililiambia Spoti Xtra kuwa: “Upo mpango wa Azam FC kuachana na Mudathir pamoja na Sure Boy ambao wamesimamishwa kutokana na utovu wa nidhamu.
Polisi Tanzania imekuwa timu ya kwanza kutuma ofa ya kuwataka nyota hao.”Spoti Xtra lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munis ili kujua ukweli wa taarifa hizo, ambapo alisema: “Mbona safi tu, kama mwalimu akiwataka hao wachezaji sisi kama viongozi tutawasajili.
“Hakuna timu ambayo haipendi kuwa na wachezaji wazuri kama hao, hususan Polisi Tanzania ambayo inataka kujiweka imara zaidi kwenye kuwania nafasi tatu za juu. Ila kwa sasa bado hakuna ripoti hiyo na timu inafanya vizuri.