MAKIPA wengi kazi yao ni kuzuia michomo kuingia ndani ya lango ila wamekuwa pia na mchango kwenye miguso ya mwisho inayosababisha kupatikana kwa ushindi kwa timu zao.
Leo tunaangazia rekodi za makipa ndani ya Bongo ambapo pasi zao zilikuwa chachu ya ushindi kwenye mechi ambazo walicheza katika mashindano tofauti:-
Nurdin Barola
Msimu wa 2020/21, Septemba 6,2020 Uwanja wa Majaliwa wakati timu ya Namungo iliposhinda bao 1-0 mguso wake ulikutana na Bigirimana Blaise dakika ya dakika ya 69 na lilikuwa ni bao la kwanza kwa msimu ndani ya ligi.
Mathias Kigonya
Kipa huyu ni mali ya Azam FC mpaka muda huu akiendelea kupambania kombe. Ilikuwa ni Mei 20,2021 wakati timu yake ya Azam FC ilipomenyana na Bashara United, Uwanja wa Azam Complex na ilishinda kwa mabao 2-0 msimu wa 2020/21.
Alitoa pasi ya bao dakika ya 10 ilikutana na muuaji anayetabasamu, Prince Dube ambaye alipachika bao hilo akiwa ndani ya 18 kwa mguu wake wa kushoto akitumia mguso uliotoka nje ya 18 kwa mguu wa kulia.
Diarra Djigui
Septemba 25,2021 Uwanja wa Mkapa Diarra alitoa mguso wa maana akiwa nje ya 18 kwa mguu wa kulia ukakutana na Farid Mussa ambaye alitoa pasi ya bao kwa Fiston Mayele.
Mayele alipachika bao lake la kwanza ndani ya ardhi ya Tanzania ilikuwa dakika ya 11 na kuwamaliza watani zao wa jadi kwa kuwa walisepa jumla na taji la Ngao ya Jamii.
Aishi Manula
Kwenye mchezo wa ligi, Oktoba Mosi, Manula alitoa mguso kwa mguu wake wa kulia akiwa nje ya 18 ukakutana na Chris Mugalu ambaye aliweza kutoa pasi ya bao kwa Meddie Kagere.
Kagere alitupia bao la kwanza ndani ya msimu wa 2021/22 dakika ya 68 kwa mguu wa kulia akiwa ndani ya 18.