MAKAMBO ATUPIA MBELE YA MLANDEGE,ZANZIBAR

HERITIER Makambo nyota wa Yanga alipachika bao pekee la ushindi katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Uwanja Aman dhidi ya Mlandege FC ya Zanzibar.

 

Katika mchezo huo dakika 45 za awali ngoma ilikuwa ngumu kwa pande zote mbili kupenya katika nyavu na kuwafanya waende mapumziko wakiwa wametoshana nguvu.

Ilibidi Yanga wasubiri mpaka dakika ya 49 kupata bao la ushindi kupitia kwa Makambo ambaye alipachika bao hilo akiwa ndani ya 18 na likajaa nyavuni.

Shuti la Fiston Mayele akiwa ndani ya 18 liligonga mwamba na kurudi ndani ya uwanja mpira huo ukakutana na Makambo ambaye alimshukuru Mayele kwa mpira wake aliopiga kwa mguu wa kulia kugonga mwamba yeye akamalizia kwa mguu wa kushoto.

Mchezo huo ni kwa ajili ya maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Bara ambazo kwa sasa zimesisimama kwa muda kutokana na mechi za kimataifa za kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Ukitazama msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi tano huku watani zao wa jadi Simba wakiwa nafasi ya pili na pointi zao ni 11.