KIWANGO CHA SAIDO CHAMUIBUA KOCHA

BAADA ya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ kucheza mechi yake ya kwanza msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi ameonekana kuvutiwa na uwezo wake.

 

 Saido alicheza mechi dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar ambapo aliingia kipindi cha kwanza akitokea benchi kuchukua nafasi ya Yacouba Songne aliyeumia.

Huo unakuwa ni mchezo wake wa kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2021/22 na Yanga iliweza kusepa na pointi tatu mazima kwa ushindi wa mabao 3-1.

Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Nabi alisema: “Ntibazonkiza alicheza vizuri, ni mchezaji mkubwa na kila mtu anafahamu hilo, ndani ya Yanga kila mtu anayo nafasi ya kucheza kama ambavyo wengine hucheza.

 

“Siwezi kusema kwa kuhakikisha atacheza katika michezo ijayo, lakini nafasi ni nzuri kwake kutokana na alichokionesha mbele ya Ruvu Shooting,”.

Yanga ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo ikiwa imekusanya pointi 15 baada ya kucheza mechi tano, imeshinda mechi zote na imefunga jumla ya mabao 9 kinara akiwa ni Feisal Salum mwenye mabao matatu na pasi moja.