>

BAO LA MK 14 LAMFANYA KOCHA AZUNGUMZE KIZUNGU

BAO la mshambuliaji wa Simba Meddie Kagere lililowapoteza Namungo FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara lilimfanya Kocha Mkuu wa Namungo FC, Hemed Morocco kuzungumza kizungu kuonesha msisitizo kwamba waliumia kupoteza mchezo huo.

Mara baada ya mchezo kukamilika na ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 1-0 Namungo, wachezaji wote wa Namungo juzi walianguka chini kwa hasira na kujilaza uwanjani kwa kuwa walikuwa wakiamini kwamba wangepata pointi mambo yakawa tofauti.

Alipoulizwa kuhusu sababu ya kufungwa kwenye mchezo huo  alijibu kifupi kwa lugha ya kizungu :”Lack of concentration,” (Kukosa umakini).

Namungo ilimaliza mchezo huo ikiwa pungufu baada ya mchezaji wake Abdulaziz Makame kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kile ambacho mwamuzi alitafsiri kwamba alimchezea faulo beki wa Simba, Shomari Kapombe.

Ushindi wa Simba unaifanya kufikisha pointi 11 ikiwa nafasi ya pili na nafasi ya kwanza ipo mikononi mwa Yanga yenye pointi 15 zote zikiwa zimecheza mechi tano.

Ilikuwa ni Novemba 3, Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo uliokuwa na ushindani mwanzo mwisho na mpaka dakika za jioni kabisa Simba ikashinda.

Ilikuwa ni kwa bao la dakika ya 90+4 ngoma ilijazwa kimiani kwa pasi ya mzawa Mohamed Hussein,’Zimbwe’.