MAPROO wa Yanga wameweka rekodi yao matata kwa kuhusika kwenye mabao mengi ya timu hiyo jambo linalowaongezea mzigo wazawa kazi ya kufanya kwenye mechi ambazo watacheza kwa msimu wa 2021/22.
Ikiwa imecheza mechi tano ambazo ni dakika 450, maproo hao wameonekana kufanya kazi kubwa kutimiza majukumu yao kuanzia kwenye safu ya ulinzi mpaka ushambuliaji jambo linaloongeza makali kwa Yanga yenye pointi 15 ikiwa nafasi ya kwanza.
Kwa upande wa kucheka na nyavu ni Fiston Mayele yeye ana mabao mawili sawa na Jesus Moloko hawa ni raia wa DR Congo na ni maingizo mapya ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.
Yacouba Songne huyu raia wa Burkina Faso ni kinara wa pasi za mwisho akiwa na pasi mbili za mabao na zote alimpa Moloko huku Djuma Shaban yeye ni beki akiwa na bao moja alilofunga kwa penalti sawa na Tonombe Mukoko.
Yanga ikiwa imefunga mabao tisa kwenye mechi zake maproo wamefunga jumla ya mabao sita huku kwa upande wa wazawa akiwa n Feisal Salum aliyetupia mabao matatu na kibindoni ana pasi moja ya bao.
Mzawa mwingine ambaye amehusika kwenye mabao ndani ya Yanga ni Farid Mussa ambaye alitoa pasi moja ya bao kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting likajazwa kimiani na Tonombe raia wa DR Congo.