MEDDIE Kagere amepachika bao la ushindi mbele ya Namungo FC dakika 90+4 kwa pasi ya Mohamed Hussein.
Bao hilo lilikuwa ni la jasho kubwa kwa kuwa Namungo walikuwa wakipambana kusaka bao kama ambavyo ilikuwa kwa Simba ambao nao walikuwa wakifanya hivyo ila mikono ya kipa Jonathan Nahimana ilikuwa kwenye ubora katika kuoka hatari.
Ni pigo la faulo ya dakika za lala salama iliyopigwa na kiungo aliyekuwa akiugua benchi Ibrahim Ajibu baada ya kuchezewa faulo na Haruna Shamte na kwa kitendo hicho Shamte alionyesha kadi ya njano.
Mzee wa Makorokocho,Ajibu ambaye alichukua nafasi ya mzee wa kukera, Bernard Morrison alitoa pasi ya upendo kwa Mohamed Hussein ambaye alimwaga majalo yaliyokutana na kichwa cha Kagere.
Katikati ya msitu wa mabeki Kagere alikwenda nao na kujaza kichwa kwenye kamba kikamshinda Jonathan ambaye alikuwa ni nyota wa mchezo katika dakika 89 ila mwisho shujaa akawa ni Kagere.
ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 11 ikiwa nafasi ya pili huku kinara akiwa ni Yanga mwenye pointi 15 wote wamecheza mechi tanotano.
Kwenye mchezo wa leo nyota wa Namungo FC, Makame Bui alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kosa la kuonekana akimchezea faulo Shomari Kapombe.