>

CAF YAMALIZA BIASHARA YA BIASHARA UNITED

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika, (CAF) limeiondoa timu ya Biashara United ya Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho kwa kutofika uwanjani kwenye mechi dhidi ya Ahly Tripoli ya Libya.

Taarifa iliyotolewa leo Novemba 3,2021 na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) imeeleza kuwa CAF imefikia hatua hiyo kwa kueleza kuwa sababu zilizoifanya timu hiyo kushindwa kufika nchini Libya hazikuwa ni za dharula hivyo biashara ya Biashara United imemalizwa na CAF.

Kwa mujibu wa barua ya CAF iliyotumwa leo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF), uamuzi wa kuiondoa timu hiyo umefanywa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho hilo.

Katika uamuzi wake, CAF imeeleza kuwa sababu zilizoifanya Biashara United kushindwa kwenda Libya kucheza mechi hiyo ya hatua ya pili ya raundi ya awali hazikutokana na dharula.Mechi hiyo ilikuwa ichezwe Oktoba 23,2021 jijini Benghazi,Libya.

Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Biashara United ilishinda kwa mabao 2-0 kwenye mechi iliyochezwa Oktoba 15,2021 Uwanja wa Mkapa.

Kwa kuondolewa kwao kimataifa sasa Biashara United wanaopenda kujiita Wanajeshi wa mpakani nguvu zao ni kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.