MARA baada ya kipyenga cha mwisho cha kumaliza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union uliochezwa
Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, baadhi ya viongozi wa Simba walivamia vyumbani na kufanya kikao kizito na wachezaji wao.
Mchezo huo ambao ulimalizika kwa suluhu, matokeo hayo hayakuwafurahisha mashabiki, wachezaji, wala viongozi hao, jambo lililolazimika kikao kizito kufanyika fasta.Hiyo ni suluhu ya pili kwa Simba msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya ile dhidi ya Biashara United, huku ikishinda 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji na Polisi Tanzania.
Spoti Xtra ambalo lilikuwepo kwenye Uwanja wa Mkapa, lilishuhudia viongozi hao wakiongozana kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji na kufanya kikao kizito.
Viongozi hao waliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salum Abdallah ‘Try Again’ ambapo katika kikao hicho, viongozi walimtaka Kaimu Kocha Mkuu, Mrundi, Thiery Hitimana kuwazuia wachezaji kurudi nyumbani na badala yake kurejea kambini kuendelea na mazoezi.
Wachezaji hao wametakiwa kila mmoja kujitathimini ili kujua sababu ya kutopata matokeo mazuri katika michezo iliyopita.
“Kiukweli kama viongozi tunaumia kutokana na matokeo mabaya ambayo tunaendelea kuyapata katika ligi, hivyo hatutaki kuona timu ikiendelea kupata matokeo haya ya suluhu.
“Hivyo leo kambi haitavunjwa na badala yake wachezaji wote watarudi kambini kuendelea na mazoezi ili kuhakikisha timu inakuwa imara.
“Tunafahamu ligi ngumu na tunakamiwa na wapinzani wetu, lakini hiyo isiwe sababu na badala yake wachezaji wanatakiwa kupambana zaidi ili tupate matokeo mazuri,” alisikika mmoja wa viongozi hao.
Akizungumzia suluhu hiyo dhidi ya Coastal, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema: “Mechi ilikuwa nzuri, kikubwa wapinzani wetu waliingia uwanjani wakiwa wamepania kwa lengo la kutafuta ushindi.
“Hivyo kama benchi la ufundi tumeyapokea matokeo hayo, tunakwenda kurekebisha sehemu zenye makosa ili katika mchezo ujao turudi tukiwa bora zaidi.”
Leo Jumatano, Simba itaikaribisha Namungo katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, mechi ikichezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.