HUU HAPA MSHAHARA KOCHA MPYA SIMBA

BAADA ya kusaini dili la miaka miwili ndani ya kikosi cha Simba, Pablo Franco raia wa Hispania anatajwa kuingia kwenye orodha ya makocha ambao watakuwa wanakunja mkwanja mrefu ndani ya Bongo ikiwa ni zaidi ya milioni 30 kwa mwezi.

 

Pablo amesaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha Simba akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Mfaransa, Didier Gomes ambaye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo Oktoba 26, mwaka huu.

 

Chanzo cha ndani kutoka Simba kimeliambia gazeti hili kuwa mkataba huo una thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani 84,000, sawa na zaidi ya shilingi Milioni 193 za Kitanzania katika vipengele vyake.

 

“Kama mnavyojua Pablo ni kocha mwenye CV kubwa sana ambaye sasa anakuja kufundisha ndani ya klabu yetu, akiwa na uzoefu wa kutosha wa soka la kimataifa alioupata akiwa nchini Hispania hususani ndani ya klabu za Getafe na Real Madrid.

 

“Hivyo hata mkataba wake ni mzito ambapo amepangiwa nyumba ya maana, usafiri na kadi ya mafuta ya kila mwezi, tiketi mbili za ndege daraja la biashara (Bussines Class) na mshahara wa dola 14,000 (zaidi ya Milioni 32 kwa kila mwezi).

 

“Lakini pia kama kocha atafanikiwa kushinda taji la Ligi Kuu basi atapata bonasi ya Shilingi Milioni 22, pesa ambayo atapata pia kama ataifikisha Simba robo fainali ya Ligi ya Kombe la Shrikisho Afrika.

“Kama timu itafika nusu fainali ya Ligi ya mabingwa (msimu ujao) basi bonasi yake itakuwa Milioni 45 na fainali atalamba Milioni 65,” kilisema chanzo hicho.

 

Mkuu wa maudhui wa Simba, Ally Shatry alisema: “Suala la kimkataba kwa taasisi yetu ni siri ya taasisi na muhusika hivyo siwezi kuweka wazi thamani ya mkataba wake.

“Lakini huyu ni kocha mwenye wadhifa mkubwa, hata yeye anaelewa mazingira ya Afrika hivyo mpaka tumefikia makubaliano ni jambo kubwa.”

Kocha huyu anatajwa kuwa alikuwa anachukua mkwanja mrefu zaidi akiwa na Getafe na Real Madrid, akiwa anapewa heshima ya kufundisha soka la kuvutia, pasi nyingi na kwake kubutua ni marufuku.

Hata hivyo, chanzo kinasema kuwa kocha huyo amewaomba Simba wawe wavumilivu kwa kipindi cha miezi miwili wakati akijaribu kuiweke timu hiyo kwenye njia anayoitaka na ataungana na Seleman Matola pamoja na Hitimana Thiery kwenye kuinoa timu hiyo.

Chanzo:Championi