>

YANGA:MOTO HUU HAUZIMI


UONGOZI wa Klabu ya Yanga umetamba kuwa moto walioanza nao kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu hauzimiki, bali wataendelea kukusanya pointi tatu katika kila mchezo ulio mbele yao ili kutimiza jambo lao la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

 

Yanga wameanza vizuri msimu huu wa 2021/22 ambapo mpaka sasa kwenye Ligi Kuu ndio vinara wa msimamo, wakiwa wamejikusanyia pointi 15 baada ya kuibuka na ushindi katika michezo yao mitano waliyocheza.

Mchezo ujao wa Yanga ni wa ugenini dhidi ya Namungo utakaopigwa Novemba 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

 Ofisa habari wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli amesema: “Kwetu sisi nguvu kubwa tumewekeza katika timu yetu kuhakikisha tunafanya vizuri katika kila mchezo ulio mbele yetu ili kufanikisha dhumuni la kushinda ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

 

“Tunajua ligi ya msimu huu ni ngumu, lakini tunajivunia ubora wa kikosi tulichonacho ambao kwa kiasi kikubwa tuna uhakika kinaweza kutimiza malengo tuliyojiwekea.”

Inakutana na Namungo ambayo imetoka kunyooshwa bao 1-0 dhidi ya Simba kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa huku Yanga ikiwa imetoka kushinda mabao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting.

Unatarajiwa kuwa mchezo utakaokuwa na ushindani mkubwa kutokana na uwepo wa washambuliaji wenye ushkaji na nyavu ndani ya Namungo ikiwa ni pamoja na Relliats Lusaje mwenye mabao mawili ndani ya Namungo sawa na Fiston Mayele wa Yanga.