KIUNGO MPYA SIMBA ANAFIKIRIA MAKOMBE

KIUNGO Mnigeria Victor Akpan ambaye ametambulishwa ndani ya Simba ameweka wazi kuwa kwa msimu ujao anaamini kuwa watashinda makombe baada ya timu hiyo kuwa na wakati mbaya msimu uliopita.

Tayari kiungo huyo ametambulishwa ndani ya Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea kikosi cha Coastal Union.

Akpan alitupia bao moja na kutoa pasi mbili ndani ya kikosi cha Coastal Union na bao lake hilo aliwafunga Simba kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani,Tanga.

Akpan amesema:”Ninajua kwamba msimu uliopita ulikuwa mbaya kwa Simba lakini sasa nina amini kwamba msimu ujao tutafanya kazi kubwa ya kuweza kupata makombe zaidi.

“Ninajiamini na nina uwezo mkubwa wa kufanya kazi hasa ukizingatia kwamba mimi ni mchezaji wa kulipwa,nimezaliwa kushinda kama ilivyo jina langu Victor ni ushindi hivyo sipendi kupoteza.

“Wengi wanapenda kucheza Simba hata mimi ilikuwa ndoto yangu ukizingatia kwamba ni timu kubwa na ina mashabiki wengi hivyo ni suala la kusubiri namna itakavyokuwa kwa wakati ujao,” .

Kwa sasa Simba imeweka kambi nchini Misri ambapo inatarajiwa kurejea kesho Bongo kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2022/23.